
Mbunge wa Jimbo la Buchosa, Eric Shigongo kupitia kwa katibu wake Julias Butogwa amekabidhi mifuko 150 ya saruji kwa wananchi wa Kijiji cha Katoma kwa ajili ya ukamilisha wa ripu pamoja na kupiga sakafu jengo la mama na mtoto katika zahati ya Kijiji hicho.

Akizungumza na wananchi kwa niaba ya Mbunge katibu ofisi ya Mbunge Jimbo la Buchosa, Julias Butogwa amesema saruji hiyo imetolewa na Mbunge kupitia mfuko wake wa Jimbo ili kukamilisha jengo hilo.

Butogwa amesema lengo la Mbunge ni kuona wananchi wa kata ya Katoma na Jimbo la Buchosa kwa ujumla wanapata huduma ya afya karibu na maeneo yao ili kupunguza vifo vya wajawazito vinavyotokea kutokana na huduma ya afya kuwa mbali na maeneo yao wanayoishi.

Aidha, ameongeza kuwa Mbunge ataendelea kutoa mchango wake wa hali na mali katika maeneo mbalimbali ya Jimbo la Buchosa katika kipindi chake cha miaka mitano ili kuondoa kero kwa wananchi wa Jimbo hilo huku akisisitiza wananchi kuendelea kujitolea kwa ajili ya kujiletea maendeleo.