
Rapa maarufu Nicki Minaj amesema kuwa mastaa wengi wa burudani wanaunga mkono mawazo yake kuhusu Donald Trump lakini wanaogopa kusema hadharani kutokana na hofu ya kukosolewa na wenzao katika tasnia ya muziki na burudani.
Katika mahojiano yake na jarida la Time yaliyochapishwa Mei 13, 2026 Minaj alisema yeye ameamua kuwa kichocheo cha mabadiliko kwa kuzungumza waziwazi kuhusu kumuunga mkono Trump.
“Wasanii wengi wanafikiri kama mimi lakini hawasemi. Wakati mwingine unahitaji mtu mmoja jasiri kubeba lawama zote,” alisema Minaj.
Msanii huyo mwenye umri wa miaka 43 alisema kwa muda mrefu alikuwa akiunga mkono Trump lakini aliogopa kuweka wazi msimamo wake kutokana na mazingira ya tasnia ya muziki ambayo, kwa mujibu wake, imejengwa kuunga mkono chama cha Democrats.

Minaj pia alimpongeza Trump kwa mvuto wake wa kipekee, akisema: “Donald Trump ana vibe yake mwenyewe,” huku akimlinganisha na Marilyn Monroe.
Katika mahojiano hayo, Minaj alimkosoa pia rais wa zamani Barack Obama pamoja na rapper Jay-Z, akidai baadhi ya rappers hawampendi Jay-Z lakini wanaogopa kusema wazi.
Aidha, Minaj alisema matukio ya “swatting” yaliyotokea nyumbani kwake Los Angeles na msaada alioupata kutoka kwa baadhi ya viongozi wa chama cha Republican ulimfanya abadili mtazamo wake kuhusu siasa na kuamua kuzungumza wazi zaidi.