×

Lwanga Apewa Kazi Maalumu Simba

MKATA umeme chaguo la kwanza la Kocha Mkuu wa Simba, Didier Gomes, Thadeo Lwanga, imebainika kwamba ana kazi maalum ndani ya kikosi hicho ndiyo maana Ijumaa hakucheza dhidi ya Al Ahly.

 

Simba ambayo juzi Ijumaa ilihitimisha hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kufungwa bao 1-0 ugenini dhidi ya Al Ahly, ilicheza mchezo huo bila ya Lwanga ambaye katika mechi tano alizocheza, alifanya kazi kubwa eneo la kiungo mkabaji.

 

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Benchi la Ufundi la Simba, Gomes aliamua kumuweka nje kabisa Lwanga akihofi a asije kuonyeshwa kadi nyingine ya njano ambayo ingemfanya akose mechi ya kwanza ya robo fainali.

 

Lwanga ambaye anaaminika kukata umeme kwenye mechi kubwa za kimataifa pamoja na zile za Ligi Kuu Bara, hivi sasa ana kadi mbili za njano, hivyo akipata ya tatu tu, basi itabidi mchezo unaofuata aukose.

“Lwanga hakuwa kabisa kwenye mipango ya kocha kwa sababu ana kadi mbili za njano, ndiye mchezaji ambaye kocha anamtegemea kwenye eneo la kiungo mkabaji.

“Endapo angecheza dhidi ya Al Ahly na ule uchezaji wake, basi kama angepata kadi nyingine ya njano, basi tungemkosa katika mchezo wa kwanza wa robo fainali kitu ambacho kocha hakutaka kitokee kutokana na kuupigia hesabu mchezo huo ambao lazima tutacheza ugenini ingawa haijafahamika itakuwa dhidi ya nani,” alisema mtu huyo.

 

Nyota huyo raia wa Uganda, kwenye mechi sita za Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi ambazo Simba imecheza, yeye ametumika kwa dakika 430 kwa mechi tano.

 

Ameikosa hiyo dhidi ya Al Ahly ugenini.Mechi ambazo alionyeshwa kadi ya njano ni dhidi ya AS Vita ugenini na Al Ahly nyumbani. Mechi nne kati ya tano alizocheza, amemaliza dakika tisini, huku moja dhidi ya Al Ahly akicheza kwa dakika 70.

LUNYAMADZO MLYUKA Dar es Salaam

Leave a Comment