
Misa maalum ya kumuombea Hayati Dk. John Pombe Magufuli, imefanyika leo katika Kanisa la Mtakatifu Petro, Oysterbay jijini Dar es Salaam ikiwa ni siku 40 tangu alipofariki dunia.
Mama Janet Magufuli, mjane wa marehemu na Mama Mary Majaliwa ambaye ni mke wa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, wameshiriki kwenye misa hiyo iliyoongozwa na mapadri wa kanisa hilo.

Mara baada ya kumalizika kwa misa hiyo, Askofu Mstaafu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Kardinali Polycarp Pengo amemtembelea Mama Magufuli nyumbani kwake na kumkabidhi zawadi ya sanamu ya Bikira Maria.

Hayati Magufuli alifariki dunia Machi 17 katika Hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam kwa maradhi ya udhaifu wa moyo aliyodumu nayo kwa takribani miaka kumi na mazishi yake yalifanyika Machi 26, 2021 Chato mkoani Geita.