
JUKWAA la muziki la Apple Music, limezindua chati mpya ya muziki iitwayo City Charts ikiwa ni moja ya majukwaa ya kwanza ya ‘kustream’ muziki mtandaoni itakayojumuisha nyimbo mpya zinazofanya vizuri katika majiji 100 duniani.

Wakati chati za kawaida zikiweka muziki kulingana na idadi ya uchezwaji wake, Apple Music City Chart inajumuisha vigezo mbalimbali vya mitaani vinavyoonesha jinsi wimbo fulani unavyokubalika katika kuorodhesha nyimbo 25 bora zinazozidi kushika kasi katika nchi husika na kuwaleta pamoja wasanii mbalimbali wanaofanya vyema duniani kote.

City Charts itakuwa ikihuishwa kila siku na itakuwa ikionekana kwenye majukwaa mbalimbali na chati za muziki za Apple sambamba na kupatikana kwa urahisi mitandaoni na kwenye vivinjari (browsers) sambamba na kwenye huduma ya kuuliza ya SIRI inayopatikana katika simu za iPhone ambapo pia msikilizaji atakuwa na uwezo wa kuongeza chati, kupakua na kusikiliza chati za miji anayoipenda kulingana na mahali alipo.

City Charts ni mwendelezo wa huduma mpya za Apple Music katika majukwaa ya muziki mtandaoni ikiwa na nyimbo zinazotamba kwenye zaidi ya majiji 100, albamu bora, nyimbo bora na chati za video za muziki zinazochezwa zaidi katika majukwaa mengine ya iTunes na Shazam.
Na Mwandishi Wetu