
Spika wa Bunge, Job Ndugai amemuonya Mbunge wa Mtama kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mhe. Nape Moses Nnauye kuchunga kauli zake anapochangia bingeni kuhusu wanawake.
Ametoa onyo hilo leo Jumatatu Mei 3, 2021 alipozungumzia mchango wa mbunge huyo kuhusu mbunge Halima Mdee na wenzake 18 waliofukuzwa uanachama Chadema lakini bado ni wabunge.
Hivi karibuni Nape alikosoa wabunge hao kuendelea na nafasi zao licha ya kufukuzwa Chadema, akitaka katiba ya nchi ifuate kumaliza hatima ya wabunge hao lakini Ndugai amesema nape hana mamlaka hayo huku akiwataka wamsamehe bure.

Nape alisema, wabunge hao wamefukuzwa Chadema, hawana sifa za kuwa bungeni. Leo Ndugai amemuombea msamaha Nape kwamba alikosea na watu wanatakiwa kumsamehe.
“Hivi karibuni mbunge wa Mtama mdogo wangu Nape Nnauye alitoa mchango wake hapa, Sina haja ya kuzuia uchangiaji wake lakini alikiuka kanuni kwa kuwataja wabunge kwa majina, hapo alikosea sana.
“Mdogo wangu Nape yalimtoka maneno kidogo na yamesambaa sana huko mitandaoni, ikifika mahali Spika na Mbunge mnapishana si jambo jema, yeye ana uhuru wa kusema lakini hana uhuru wa kuwasema wabunge wenzake, nilizungumza nae na ninawaomba mumsamehe, aliwakosea sana na ninaomba sana tuchunge midomo yetu.
“Nape (Nnauye) alikosea kuwasema vibaya (Halima Mdee na wenzake 18), lakini Nape mdogo wangu, unaposhughulika na wanawake, ongea nao kwa heshima na hiyo iko hivyo dunia nzima,” amesema Spika Ndugai.