×

Dkt. Abassi: Peak Time Wamerudisha Hadhi Ngumi Nchini

MABONDIA na wadau wa mchezo wa ngumi za kulipwa juzi Jumapili waliweza kujumuika katika futari ilioandaliwa na Kampuni ya Peak Time Sports Agency ambayo imekuwa kiandaa mapambano mbalimbali ya ngumi huku mgeni rasmi akiwa ni Katibu mkuu wa Wizara ya Habari Sanaa, utamaduni na michezo, Dkt. Hassan Abassi.

 

Katika tukio la futari hiyo ambayo imefanyika kwenye Ukumbi wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania Club 361 uliopo Lugalo, Mwenge iliweza kuhudhuriwa na wageni mbalimbali akiwemo Shekhe mkuu wa mkoa wa Alhad Mussa Salum.

Kupitia futari, mkurugenzi wa kampuni ya Peak Time Sports Agency, Kapteni Seleman Semunyu ameiomba Serikali kuwaongeza nguvu waandaji wa mapambano ili kuweza kupata wadhamini wa kubwa pamoja kumuomba Waziri mkuu , Kasim Majaliwa kukubali ombi la kuwa mgeni rasmi katika pambano kati ya Dullah Mbabe na Twaha Kiduku litakalo fanyika Julai 24, mwaka huu.

Kwa upande wa mgeni Rasmi, Dk Hassan Abassi alisema kuwa: “Kipekee tumshukuru mtu kama Semunyu na Peak Time ambao wamerudisha hadhi ya mchezo huu lakini nimemuona ndugu yangu Jay Msangi na wengine, nafikiri tangu enzi zile za kina Tyson baadaye mchezo wa ngumi ukapotea, hawa watu na wengine wamerejesha hadhi ya mchezo wa ngumi Tanzania, tuwashukuru sana.

“Lakini kabla ya kuendelea nimechomekewa mambo kadhaa hapa na shekhe Semunyu sasa tumalizane hapa hapa ila tukubaliane kwamba iwe hivyo hii futari iendelee kila mwaka.

“Unajua watu wa michezo siyo watu poapoa, hususani mabondia siyo watu wa kushindwa, nafikiria adhimio la kwanza futari hii iwepo na wenyeji ni mabondia.

 

“Lakini ambacho naweza kusema kwa niaba ya wizara na kwa niaba ya serikali, sisi wizara tunaanza kuondoka kuwa watazamani/ wasimamizi wa sera, nawaahidi kwamba tunaenda kuwa mapromota siyo kwenda kunyang’anya wengine hapa ila tupo kwenye juhudi za kwenda kusaidia michezo.

“Inapotokea matukio makubwa kama haya ambayo watu wamebuni, wamewaza, wakaweka wamazo yao katika utekelezaji, nawahidi kwamba wizara yenu ya habari inaenda kubadilika na kuwa ya kufanya mikakati ambayo itaweza kushiriki kwa kutia chochote kitu kwenye kuwezesha michezo mbalimbali na lile ombi la waziri mkuu nimelichukua,” alisema Dk Abassi.

Leave a Comment