×

Museveni Aapishwa Kuwa Rais wa Uganda

Rais wa Uganda Yoweri Museveni ameapishwa kuongoza nchi hiyo kwa kipindi cha sita, miaka 35 baada ya kuchukua hatamu kama rais.

Museveni alishinda uchaguzi uliokumbwa na utata dhidi ya mpinzani wake Bobi Wine na hivi leo akaapishwa ili kuhudumu kwa kipindi cha sita kwenye hafla iliyoandaliwa katika Bustani ya Kololo, Jijini Kampala.

 

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta ni miongoni mwa takriban viongozi 11 wa mataifa mbali mbali waliohudhuria hafla hiyo.

Rais Kenyatta, ambaye ndiye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ameandamana na mawaziri Raychelle Omamo (wa maswala ya nje), Peter Munya (wa Kilimo) na James Macharia (wa Uchukuzi).

 

Viongozi wengine waliohudhuria hafla hiyo ni pamoja na Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania , Évariste Ndayishimiye wa Burundi, Mohamed Abdullahi Mohamed wa Somalia, Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe, Salva Kiir wa Sudan kusini , Hage Gottfried Geingob wa Namibia, Alpha Conde wa Guinea, Félix Antoine Tshisekedi Tshilombo wa Jamhuri ya Congo pamoja na Nana Addo Dankwa Akufo-Addo wa Ghana.

Museveni, aliye na umri wa miaka 77, alichukua hatamu ya uongozi kwa mara ya kwanza nchini humo mwaka 1986 na kuwa rais wa tisa wa Uganda.

Leave a Comment