
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akipokea Ripoti ya Kamati Maalum aliyoiunda kwa ajili ya kufanya tathmini ya Ugonjwa wa Corona COVID -19 nchini kutoka kwa mwenyekiti wa kamati hiyo Prof. Said Aboud Ikulu Jijini Dar es Salaam leo tarehe 17/5/2021.
Kamati hiyo imesema kuwa chanjo dhidi ya ugonjwa huo ni salama na zimeonesha ufanisi. Akizungumza wakati wa kukabidhi ripoti hiyo, mwenyekiti wa Kamati hiyo, Prof. Said Aboud amesema;
“Tangu kuingia kwa Covid 19 Tanzania March 2020, Tanzania imekumbwa na mawimbi mawili makubwa na sasa kutokana na mwenendo wa ugonjwa huo katika Mataifa mengine Duniani, kuna tishio la kutokea wimbi la tatu nchini.
“Chanzo ya COVID-19 itolewe kwa vipaumbele kwa kuanzia kwa wahudumu wa afya, watumishi wa umma, viongozi wa dini na mahujaji, wazee, wenye maradhi sugu, watumishi wa vyombo vya ulinzi na usalama na wasafiri wanaokwenda nje ya nchi.
“Kamati inaishauri serikali kwa kutumia vyombo vyake iendelee na hatua kuelekea kuruhusu matumizi huru ya chanjo dhidi ya COVID-19 kwa kutumia chanjo zilizoorodheshwa na WHO ili kuwapa fursa ya kinga wananchi wake.
“Kamati imebaini kuwa mwamko wa kudhibiti wimbi la kwanza la Corona ulikuwa mkubwa ukilinganisha na wimbi la pili, Kamati imeshauri kuimarisha kasi kudhibiti tishio la wimbi la tatu.
“Baada ya uchambuzi wa kina Kamati imependekeza Serikali itoe taarifa juu ya uwepo wa ugonjwa wa Covid 19 na ichukue hatua madhubuti kuimarisha hatua zote za kinga katika ngazi zote ili kuepusha wimbi la tatu la ugonjwa huo.
“Tanzania ishiriki ipasavyo katika maamuzi na itekeleze maazimio ya Kikanda na Kimataifa iliyoridhia katika Jumuiya za Afrika Mashariki, SADC, AU na WHO.
“Kuhusu chanjo dhidi ya Covid 19, Kamati inashauri Serikali kupitia vyombo vyake iendelee na hatua kuelekea kuruhusu matumizi huru ya chanjo dhidi ya Covid 19 kwa kutumia chanjo zilizoorodheshwa na WHO ili kuwapa fursa ya kinga Wananchi wake.
“Kipaumbele cha utoaji wa chanjo ya Corona kiwe kwa Watumishi walio mstari wa mbele wa utoaji wa huduma mathalani Watumishi wa Sekta ya Utalii, Hoteli, Mipakani, Viongozi wa Dini na Mahujaji, Wazee, Watu wazima kuanzia miaka 50 na wenye maradhi sugu.
“Kipaumbele cha utoaji wa chanjo ya Corona kiwe kwa Watumishi wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama na Wasafiri wanaokwenda nje ya Nchi, pia kufanya uhamasishaji na maandalizi ya upokeaji, usafirishaji na utoaji wa chanjo na Wananchi wawe huru kuamua kuchanja au laah.
“Serikali itumie fursa zilizipo wakati huu wa janga la Covid-19 kuanza mchakato wa uanzishaji wa viwanda vya kutengeneza chanjo, Serikali iimarishe huduma za uchunguzi kwa kuijengea uwezo Maabara ya Taifa na Maabara nyingine ili kupanua wigo wa upimaji wa Corona.
“Serikali itoe takwimu sahihi za ugonjwa wa Covid-19 kwa Umma na WHO ili Wananchi wapate taarifa sahihi kutoka Mamlaka za Serikali na kuheshimu makubaliano na kanuni ambazo Nchi iliridhia.
“Serikali iendelee kuhakikisha kuwa matumizi ya tiba asili na tiba mbadala katika mfumo rasmi wa tiba za kisasa yanazingatia mifumo ya kisayansi.
“Serikali iendelee kuzingatia mazingira ya Kitanzania katika udhibiti wa Covid 19 katika kuamua kuweka au kutoweka shuruti ya kujifungia (lockdown) na kuwa na ubunifu ili kuruhusu ukuaji wa uchumi na kuimarisha sekta zinazochangia uchumi,” amesema Prof. Said Aboud.