
WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi wa Uganda Jenerali Katumba Wamala ametoa shukran zake kufuatia shambulio lililomlenga Jumanne asubuhi, akimshukuru Mungu kwa kunusurika na shambulio hilo.
Katika ujumbe alioutoa katika video fupi iliyorekodiwa kutoka katika Hospitali ya Medipal Katumba ambaye pia ni amesema: ‘’Mungu amenipa nafasi ya pili, nitakuwa vyema tena msiwe na wasiwasi, sina majeraha mabaya, ni mikono tu, lakini nitakuwa sawa.
Niko na madaktari na wanafanya kila liwezekanalo, nawapenda nyie watu, Tafadhali muombeeni mama, yuko katika hali mbaya’’.
Binti yake Wamala Brenda Nantongo, na dereva waliuawa katika shambulio lililofanywa na wanaume wanne ambao walikuwa kwenye pikipiki.
‘’Nimenusurika, lakini binti yangu Brenda Nantongo Katumba na dereva wangu Haruna walikufa katika eneo la tukio. Sijui sababu ya shambulio hili. Hapakuwa na sababu ya kumaliza maisha ya watu wasio na hatia.
Roho zao zipumzike kwa amani’’, ujumbe wa Twitter wa Jenerali Wamala ulisema.
