
Mapato ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) yameongezeka kutoka kukusanya Sh72 bilioni mwaka 2016 hadi Sh160 bilioni mwaka 2020/2021 na limeacha kutegemea ruzuku kutoka serikalini.
Kauli hiyo imetolewa leo Jumatano, Juni 2, 2021 bungeni na Waziri wa Nishati Dk Medard Kalemani wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa Fedha 2021/2022.
Waziri Kalemani amesema ongezeko hilo ni sawa na asilimia 102 na limetokana na matumizi ya mfumo wa Lipa Umeme Kadri Unavyotumia (LUKU) unaotumika kwa wateja wote nchini.
“Kuongeza kasi ya kufuatilia madeni sugu ya wateja wa Tanesco na kupungua kwa madeni haya kutoka Sh272 bilioni mwaka 2017 kufikia Sh48.9bilioni mwaka 2020.
Dk Kalemani amesema Shirika la Tanesco hivi sasa linaendesha shughuli zake kwa kujitegemea bila kupata ruzuku ya Sh143 bilioni ilizokuwa ikizipata kila mwaka kutoka serikalini.