×

Injinia: Yanga Tunafanya Usajili Mkubwa

UONGOZI wa Klabu ya Yanga umetamba kuwa, upo kwenye mipango mizito ya kukisuka upya kikosi chao kitakachofanya vizuri na kuandika rekodi mpya katika michuano ya Afrika, mwakani.

 

Katika kufanikisha hilo, uongozi wa Kampuni ya GSM ambao ni wadhamini wa klabu chini ya Mkurugenzi wa Uwekezaji ambaye pia Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano na Usajili, Injinia Hersi Said wamefunguka kujipanga vizuri kuhakikisha wanatimiza hilo.

 

Yanga hadi hivi sasa wamefanikisha usajili wa mastaa watatu ambao ni Shaaban Djuma wa AS Vita, Dickson Ambundo anayekipiga Dodoma Jiji na David Bryson wa KMC FC huku pia wakiwa kwenye mazungumzo ya kumrejesha nchini Straika, Heritier Makambo aliyebakisha mkataba wa mwaka mmoja Horoya AC ya nchini Guinea.

 

Akizungumzia mipango ya usajili ya Yanga, Hersi alisema: “Tunajivunia mafanikio makubwa ambayo kikosi chetu kimekuwa nayo msimu huu, na ni wazi hili linatokana na usajili bora ambao tuliufanya mwanzoni mwa msimu.

“Kama utafanya tathimini basi utagundua kuwa kati ya wachezaji 16 ambao tumewasajili msimu huu, ni wachezaji wasiozidi watatu ndiyo ambao wameshindwa kuwa na mchango mkubwa kwenye kikosi na pia ni kwa sababu mbalimbali.“Na niseme kuwa hatujamaliza kuijenga timu, msimu ujao tutafanya usajili mkubwa wa wachezaji bora, ili kutimiza adhima yetu ya kurudi juu katika michuano ya Afrika. Tunaandaa kikosi bora kitakachoweza kufanya hivyo.

 

KUHUSU MAENDELEO YA KLABU

“Tuna furaha na maendeleo ambayo klabu yetu imeyapata mpaka sasa, kulinganisha na misimu miwili au mitatu nyuma. Tumekuwa na maendeleo makubwa katika maeneo kadhaa kama vile ustawi wa kiuchumi, kiutendaji, usajili na ubora wa wachezaji bila kusahau kwenye uongozi.

 

THAMANI YA YANGA

“Kuelekea mkutano wetu mkuu utakaofanyika Juni 27, mwaka huu tunatarajia baada ya kukubaliana katika masuala ya mabadiliko ya kiuendeshaji wa timu yetu, utafuatia mchakato wa kuithaminisha klabu yetu, na naamini thamani ya klabu hii ni kubwa kuliko klabu yoyote hapa nchini.

 

KUHUSU KUFUKUZA MAKOCHA

“Nisingependa kuongea sana kuhusu mapungufu ya wakufunzi wetu waliopita kuanzia kwa Zlatko Krimpotic mpaka Cedric Kaze, nachoweza kusema ni kwamba maamuzi yaliyofanyika juu ya makocha wetu yalikuwa sahihi, na kwa maslahi mapana ya klabu.

KUHUSU UBORA WA SIMBA KWA SASA

“Simba tayari wako kwenye mafanikio, Yanga wako kwenye mchakato wa kwenda kwenye mafanikio, wanaonyesha kiwango kizuri sana, na ni jambo zuri kwao kama klabu.“Lakini niweke wazi kuwa sisi tumewaacha mbali sana, na wala hatujifananishi na Simba kwa kuwa Yanga ni taasisi tofauti. Kila mtu anajua unapozungumzia suala la mafanikio, basi Yanga ndiyo timu inayozungumzwa zaidi kwa Tanzania.

 

ISHU YA UBINGWA MSIMU HUU

“Yanga ni timu kubwa na naweza kusema sisi hatupo kuwasindikiza wengine, ni kweli nilisema kuhusu ishu ya ubingwa msimu huu, tayari tumefanikiwa kushinda ubingwa wa Kombe la Mapinduzi.

 

Tunakwenda kucheza nusu fainali ya Kombe la Shirikisho na tutafika fainali na tutamfunga yeyote tutakayekutana naye fainali, iwe ni Simba au Azam FC na kutwaa kombe hilo.“Kuhusu Ligi Kuu Bara, mpaka sasa tupo kwenye nafasi ya pili kwenye msimamo na tuna nafasi ya kushinda ubingwa msimu huu.“Kama uongozi tumeweka wazi kwa watendaji wote wa klabu kuwa unapohusika na Yanga ni lazima uwaze kutwaa ubingwa na si vinginevyo.

 

KUHUSU UJIO WA MANJI

“Sisi kama GSM, hatuna shida yoyote na mtu anayetaka kuisaidia Yanga kupitia uwekezaji, na mara zote tumekuwa tukisema hivyo, si tu kwa Manji bali yoyote anayetaka kuisaidia Yanga katika uwekezaji anaruhusiwa kuja

Stori: Joel Thomas na Wilbert Molandi,Dar

Leave a Comment