
GIFTY Stanford a.k.a Gigy Money; ni msanii wa kike wa Bongo Fleva ambaye mbali na kutoa burudani, pia amekuwa na vimbwanga kama vyote.Gigy ambaye takriban miezi sita alikuwa amefungiwa kufanya sanaa na Baraza la Sanaa Taifa (Basata) kutokana na kusambaa kwa video yake iliyodaiwa ni chafu akiwa jukwaani amefanya mahojiano maalum na Gazeti la IJUMAA na kueleza shauku yake ya kumfanya mwanawe, Mayra afanane na yule wa mwigizaji Irene Uwoya aitwaye Krish Ndikumana;
IJUMAA: Hongera Gigy kwa kufunguliwa na Basata.
GIGY: Asante sana maana kufungiwa siyo mchezo jamani, watu wasikie tu hivyohivyo nakuambia.
IJUMAA: Mara nyingi kwenye kurasa zako za mitandao ya kijamii umekuwa ukiweka ujumbe wa jinsi unavyotamani kufanya sherehe ya mtoto wako iwe kubwa na nzuri, lakini hata pesa ya kumpiga picha ilisumbua, hii unaizungumziaje?

GIGY: Ni kweli nilikuwa napitia kipindi kigumu sana, lakini siyo kwamba nilikuwa sili au kufanya vitu vyangu vingine, ila tu hata mimi nilitamani kumfanyia mwanangu Mayra kitu kikubwa kama Uwoya alivyomfanyia Krish sherehe ya komunio, lakini haikuwezekana, mambo yalikuwa magumu mno.
IJUMAA: Kwa hiyo ulikuwa ukijikimu maisha yako na nini au ulipata msaada zaidi kutoka kwa baba wa mtoto wako?
GIGY: Mambo ya baba mtoto siyataki maana hanisaidii kitu kabisa, hata kidogo, nilikuwa najikimu kutokana na mambo mengine ninayofanya.
IJUMAA: Kwa nini umesema ulitamani kumfanyia mwanao kama Uwoya alivyomfanyia mwanawe?
GIGY: Hivi huoni sherehe ilivyopendeza na ni kubwa sana? Sitaki kabisa mtoto wangu apitie maisha niliyoyapitia mimi kwa sababu siyo mazuri.
IJUMAA: Ulipopata adhabu ya kufungiwa kuna kitu chochote umejifunza?
GIGY: Sana, jamani nikae miezi sita bila kufanya kazi, kwa nini nisijifunze kitu? Unajua kuna wakati mwingine sisi tunapenda zaidi kufurahisha watu na mashabiki wainjoi ndiyo inatukosti.
IJUMAA: Kipindi ambacho ulifungiwa kuna kazi ambazo ulikuwa ukitengeneza?
GIGY: Nyingi sana na nzuri mno, siku nikiziachia kila mtu atashangaa kwa kweli.
IJUMAA: Japokuwa ulikuwa kwenye kipindi kigumu sana, lakini muonekano wako ni wa kuvutia na kupendeza, ni nini siri yako?
Gigy: Mimi ni mrembo mno, pamoja na yote najitahidi sana kujitengeneza kwani umaridadi huficha umaskini siku zote na ndiyo maana huwezi kunikuta ninanuka jasho wala nywele zangu chafu kwa sababu najipenda sana.
IJUMAA: Hivi karibuni ulikuwa ukimnadi mpenzi wako mpya, hii huoni kama huwa inakuletea matatizo maana mara nyingi hamuishii vizuri?
GIGY: Yaani ni kwamba ninapomposti mpenzi wangu ninaonesha ujasiri maana nikimficha ili iweje? Bora aonekane na anayemuiba ajue kabisa anachukua mali ya Gigy, hapo ndipo tunapoanzia.
IJUMAA: Hivi karibuni Amber Lulu alikutana na kadhia kubwa kuhusiana na watu kumkosoa mtoto wake, wewe kama mama na msanii mwenzako unasemaje?
GIGY: Kwanza nilikereka sana na tukio hilo kwa sababu Amber ni mtu wangu wa karibu, halafu yule ni malaika wa mbinguni tu jamani, wanataka nini lakini? Niliumia sana tena sana.
IJUMAA: Hivi bifu lako na Amber Lulu liliishia wapi?
GIGY: Sisi hatuna bifu, yule ni mtu wangu wa karibu kuliko yeyote yule na ni mshauri wangu ‘so’ hatuna mabifu ya kuendelea.
IJUMAA: Haya asante sana Gigy kwa ushirikiano wako.GIGY: Tupo pamoja, karibu tena na tena
Stori: IMELDA MTEMA, DAR