
UNAAMBIWA nahodha wa Simba, John Bocco, amepambana kadiri ya uwezo wake kuhakikisha anambakiza kikosini hapo beki wa kushoto wa timu hiyo, Gadiel Michael, jambo lililowafanya mabosi hao kuachana na usajili ya David Luhende.
Simba ilikuwa kwenye rada kali za kusaka beki wa kushoto mzawa, ili aweze kusaidiana na nahodha msaidizi wa kikosi hicho, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, ambapo walianza na Charles Manyama wa Ruvu, wakapigwa bao na Azam FC, kisha wakahamishia nguvu kwa Luhende ambaye naye wameachana naye.
Chanzo chetu kutoka ndani ya Simba, kimelinyetishia Championi Jumamosikwamba, juhudi za Bocco za kuwaomba mabosi wa usajili na kocha wao Didier Gomes Da Rosa, wambakize Gadiel Michael, zimefanikiwa ambapo sasa atapewa mkataba mpya.

“Taarifa zilizopo katika kamati ya usajili na Bodi ya Wakurugenzi ilikuwa ni kupitia ripoti ya kocha ambapo tayari kuna wachezaji hawataondolewa na miongoni mwao ni Gadiel, ambaye yeye amenusurika zaidi baada ya Bocco kuulizwa na viongozi kama aondoke au la ambapo alipendekeza abaki.”
Championi lilimtafuta Mkuu wa Maudhui wa Simba, Ally Shatry ‘Bob Chico’, ili azungumzie hilo, ambapo alisema:
“Kwa sasa siwezi kukuambia kitu maana sijapata mrejesho baada ya kikao cha bodi, hivyo suala lote la usajili litafahamika baada ya kupewa maelekezo na uongozi au kocha.”
STORI: MUSA MATEJA, Dar es Salaam