YANGA inatajwa kumalizana na kiungo mshambuliaji na nahodha wa Gor Mahia ya Kenya, Kenneth Muguna kwa kumpa mkataba wa miaka miwili.Muguna mwenye umri wa miaka 25, akiwa na Gor Mahia alikuwa akicheza namba 10 pacha na Jacques Tuyisenge wakiunda safu ya ushambuliaji ya timu hiyo.
Yanga imepanga kuifanyia maboresho safu hiyo ya ushambuliaji kwa kusajili majembe ya maana kuelekea msimu ujao ambapo watashiriki michuano ya kimataifa.
Mmoja wa mabosi wa timu hiyo, ameliambia Spoti Xtra, kuwa kiungo huyo tayari yupo Tanzania na Jumamosi alikuwepo kwenye Uwanja wa Mkapa kushuhudia Kariakoo Dabi ambayo Yanga iliifunga Simba bao 1-0.
Bosi huyo alisema, usajili wa mchezaji huyo na wengine nane umefanywa kwa siri kubwa kwa hofu ya kutibuliwa na wapinzani wao Simba na Azam FC.“Kwa asilimia kubwa Yanga wamemalizana na Muguna, kiungo mshambuliaji wa Gor Mahia kwa mkataba wa miaka miwili.
“Muguna yupo nchini tangu wiki iliyopita, amewekwa kwenye moja ya hoteli kubwa hapa Dar akiendelea kupatiwa huduma nyingine na juzi alikuwepo kwenye Uwanja wa Mkapa akifuatilia Kariakoo Dabi.“Uwanjani hapo alikuwa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Injinia (Hersi Said) wakifuatilia mchezo huo,” alisema bosi huyo.
Injinia Hersi hivi karibuni aliliambia Spoti Xtra kuwa: “Yanga ikiwa chini ya GSM tutafanya usajili bora kwa kumsajili mchezaji yeyote kwa pesa yoyote ili kuhakikisha tunaijenga timu itakayokuwa tishio na mfano wa kuigwa Afrika.”
STORI: WILBERT MOLANDI
