WAGHANA wa Yanga, Michael Sarpong na Lamine Moro, wanatarajiwa kuingia kambini kuungana na wachezaji wenzao mara baada ya mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Ihefu FC.
Mastaa hao waliondolewa kambini hivi karibuni kwa kile kilichotajwa utovu wa nidhamu waliouonyesha wakiwa na timu hiyo kabla ya Kocha Mkuu Nasreddine Nabi kuwatimua. Wachezaji hao walikosa michezo kadhaa ya ligi na Kombe la FA waliyoicheza kutokana na kutumikia adhabu hiyo ya kuondolewa kambini.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Yanga, Dk Mshindo Msolla, wachezaji hao wanatarajiwa kuwa sehemu ya kikosi kitakachocheza mchezo wa fainali ya FA dhidi ya watani wao Simba utakaopigwa Julai 25, mwaka huu kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika.
Msolla alisema kuwa wachezaji hao wamerejeshwa kambini baada ya kukiri kufanya utovu wa nidhamu mbele ya kamati yao ya nidhamu katika kikao chao walichokaa Jumamosi iliyopita kabla ya kurejeshwa kikosini.Aliongeza kuwa wachezaji hao wameondolewa kwenye mipango ya mchezo wao watakaoucheza kesho Alhamisi dhidi ya Ihefu kutokana na kutokuwepo kambini kwa muda mrefu.
“Moro na Sarpong wataingia kambini rasmi baada ya mchezo wetu wa ligi dhidi ya Ihefu tukiwa tunajiandaa na fainali ya FA tutakayocheza dhidi ya Simba.“
Katika mchezo huu dhidi ya Ihefu kocha amewaondoa katika mipango yake kuto–kana na kutokuwepo kam–bini kwa muda mrefu,” alisema Msolla.KUHUSU METACHAAidha uongozi wa Yanga umepanga kukutana na menejimenti ya kipa wao Metacha Mnata kwa ajili ya kufanya ma–zungumzo ya mwisho kwa ajili ya kumuongezea mkataba mpya wa kuendelea kukipiga Jang–wani.
Hiyo ikiwa siku imepita tangu kipa huyo arejeshwe kambini kwa ajili ya kuanza maandalizi ya mchezo wa Fainali ya Kombe la FA dhidi ya Simba utakaopigwa Julai 25, mwaka huu kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma.Kipa huyo hivi karibuni aliondolewa kambini wakati timu hiyo ikiwa mkoani Dodoma ikijiandaa na mchezo wake wa Ligi Kuu Bara dhidi ya JKT Tanzania.
Kwa mujibu wa Msolla, kipa huyo anatarajiwa kumaliza mkataba wake mwanzoni mwa Agosti, mwaka huu.“Ninafahamu uwezo mkubwa alionao Metacha, hivyo tumepanga kumuongezea mkataba mpya wa kuendelea kuichezea Yanga katika misimu mingine.
“Atasaini mkataba huo mara baada ya kufikia muafaka mzuri na menejimenti yake inayomsimamia, tunamuongezea mkataba baada ya kukiri kufanya makosa kutokana na utovu wake wa nidhamu alioufanya kwa mashabiki.”
WILBERT MOLANDI NA SAID ALLY, Dar
