×

Maumivu Kodi Mpya Miamala ya Simu, Vilio Kila Kona

NI maumivu, ndivyo unavyoweza kueleza kilio kilichojitokeza kwa baadhi ya watumiaji wa simu za mkononi nchini baada ‘kodi ya uzalendo’ kuanza kukatwa kwa wanaotuma au kutoa fedha kwa wakala wa simu za mkononi.

 

Hatua hiyo imekuja baada ya Juni mwaka huu Bunge kuidhinisha tozo ya Sh10 hadi Sh 10,000 katika miamala ya kutuma na kutoa pesa kwenye bajeti yake ya Sh36.33 trilioni ya mwaka wa fedha wa 2021/22.

 

KILIO

Baadhi ya watumiaji wa huduma hizo wameeleza kushtushwa na kiwango kikubwa cha makato ya tozo hiyo ambayo kwa tathmini ya awali inaonesha kuwa serikali inachukua kiwango kikubwa kuliko hata kampuni za simu zinazotoa huduma hiyo.

 

Mmoja wa wananchi hao ni Thadeo Mushi alisema tozo hiyo itapunguza kiwango cha miamala kwenye mitandao ya simu hivyo kusababisha Serikali kupata hasara badala ya faida.Mushi alisema watu watakimbilia kupata huduma za benki kutuma au kutoa fedha jambo ambalo litarejesha misongamano kwenye benki.

 

Hoja hiyo ya Mushi iliungwa mkono na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuendeleza Huduma za Fedha Tanzania (FSDT), Sosthenes Kewe ambaye alisema mabadiliko haya mapya, mteja wa miamala kwa simu ya mkononi atakuwa analipa kodi tatu.

 

Kwanza ni ushuru wa forodha ambao ni asilimia mbili na asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT). Hizi mbili zilikuwepo kabla ya mabadiliko yanayoanza leo.

 

WASOMI

Wakati Mushi na Kewe wakisema hayo, Profesa wa uchumi, Haji Semboja alisema haoni tatizo kwani jambo la msingi ni pesa hizo kuenda kwenye matumizi sahihi.

 

Hata hivyo, alitoa tahadhari kwa watanzania kuhamia katika masafa mengine ya simu ili kupata huduma za chini za miamala hiyo. Hoja hiyo iliungwa mkono na Mbunge wa Kinondoni, Tarimba Abbas –CCM ambaye alisema wabunge watakuwa wakali kwa wabadhirifu wa fedha zitakazotokana na kodi hiyo.

 

HALI ILIVYO

Kabla ya kodi ya uzalendo, wateja wa Airtel Money walikuwa wanakatwa shilingi 350 tu ndani ya mtandao kutuma shilingi 15,000, lakini sasa watalipa shilingi 960 na walikuwa wanakatwa shilingi 550 kwenda mtandao mwingine, lakini imepanda mpaka shilingi 1,160.

 

Watakapotaka kutoa, watalipia shilingi 2,010 badala ya shilingi 1,400 ya mwanzo.

Kwa wateja wa Mpesa, kutuma shilingi 15,000 kwenda kwa mteja asiyesajiliwa, makato yatakuwa shilingi 970 kutoka shilingi 360 wakati ikigharimu shilingi 2,820 kwa mteja asiyesajiliwa kutoka shilingi 2,210.

 

Kwenda mitandao mingine, kiasi hicho kitalipiwa shilingi 1,160 kutoka shilingi 550 iliyokuwapo na watakaopelekwa kwenye akaunti zao za benki watakatwa shilingi 1,810 badala ya shilingi 1,200 iliyokuwapo.

 

Kutoa kiasi hicho iwe kwa wakala au ATM, watakatwa shilingi 2,060 kutoka shilingi 1,450.

 

WAZIRI

Akizungumza kwenye kipindi cha 360 cha kituo cha runinga cha Clouds, Julai 12, mwaka huu, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba alisema; “Hii siyo tu ni kodi bali tunatunisha mfuko wa mshikamano.

 

Tutachangia kupitia makato ya simu.”Waziri huyo alisema itakuwa aibu kwa miradi ya maendeleo kukwama kwa kuwa tu Serikali imeshindwa kukusanya kodi hivyo akavitaka vyombo vya habari kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kodi kwa maendeleo yao.

 

View this post on Instagram

 

A post shared by Global Publishers (@globalpublishers)

Leave a Comment