×

Polisi Yakiri: Tunamshikilia Mbowe, Anahojiwa

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limethibitisha kumshikilia Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe kwa mahojiano.

 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ramadhani Ng’anzi amesema kiongozi huyo wa chama kikuu cha upinzani nchini alitiwa mbaroni alfajiri ya kuamkia jana Jumatano Julai 21, 2021 akiwa katika Hoteli ya Kingdom, Mtaa wa Ghana jijini humo.

 

Kamanda Ng’anzi, amesema baada ya kumkamata, alisafirishwa mpaka jijini Dar es Salaam ambako polisi walisema walikuwa wakimtafuta kwa makosa mengine anayodaiwa kuyafanya ambako mpaka sasa anaendelea kuhojiwa.

 

“Baada ya kumkamata, wenzetu wa Dar es Salaam nao walitueleza kuwa wanamtafuta kwa makosa mengine anayodaiwa kuyafanya huko; hivyo tulimsafirisha kwenda Dar es Salaam anakoendelea kuhojiwa,” amesema Kamanda Ng’anzi.

 

Amesema kiongozi huyo wa Chadema hivi sasa yuko kwenye mikono salama ya polisi Mkoa wa Dar es Salaam na atarejeshwa Mwanza baada ya mahojiano ili aunganishwe na wenzake 15 wanaoshikoliwa kuhusiana na kongamano la Katiba Mpya lililozuiwa na jeshi hilo jana.

 

Leave a Comment