
Mwanamuziki Waziri Ally Seif aliyefariki juzi usiku, amezikwa Pongwe, Tanga leo Julai 25, 2021 huku mamia ya watu wakishiriki mazishi hayo.
Kuanzia asubuhi umati mkubwa wa watu ulikuwepo barabara ya 21 Tanga mjini nyumbani kwa kina Waziri Ally kushiriki taratibu zote muhimu ikiwemo swala ya jeneza na ilipotimu saa 5 kamili, safari ya kuelekea Pongwe kwenye mazishi ikaanza.

Waziri Wizara ya Nchi,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Ummy Mwalimu na Mbunge wa jimbo la Muheza, Hamisi Mohammed Mwinjuma (Mwana FA) ni miongoni mwa viongozi walioshiriki msiba wa Waziri Ally.
Ally Kileo, Juma Mbizo, Abdallah Fereshi, Faza Luzozi, Ibony Moalim na Henry Mdumu, ni baadhi tu kati ya wadau wengi wa muziki waliofunga safari kutoka Dar es Salaam kuja Tanga kumzika Waziri Ally.
Hadi ilipotimu saa 6.15 mchana tayari mwili wa Waziri Ally ambao ulikuwa haukauki tabasamu usoni mwake, ukawa umeshahifadhiwa kwenye makazi yake ya kudumu, Pongwe nje kidogo ya jiji la Tanga.
PICHA/STORI NA SAID MDOE
