×

Aliyetakiwa na Luis Simba Atua Yanga Usiku

TAYARI Yanga imefanikiwa kumnasa kiungo mshambuliaji wa UD Songo ya Msumbiji, Jimmy Julio Ukonde kwa ajili ya msimu jao wa Ligi Kuu Bara na michuano ya kimataifa, huku ikielezwa kuwa Luis Miquissone alimtaka Simba.

Kiungo huyo ametua nchini juzi usiku, licha ya ujio wake kufanywa siri lakini tayari ameanza maisha mapya ndani ya kikosi hicho kabla ya mchana wa juzi Yanga kumpokea mshambuliaji kutoka AS Vita, Fiston Mayele raia wa DR Congo.

Ukondo ambaye ndiyo alikuwa pacha wa kiungo mshambuliaji wa Simba, Luis Miquissone, amewahi kuja nchini ikiwa ni lengo la nyota huyo mwenye urefu wa mita 1.60 akiwa na uwezo wa kucheza nafasi ya kiungo wa kati na kiungo mshambuliaji.

Hata hivyo, taarifa zinasema kuwa Luis aliwahi kuwashauri Simba wamsajili mchezaji huyo kutokana na ubora ambao amekuwa akiuonyesha uwanjani.

“Luis aliwahi kumzungumzia siku moja huyu mchezaji na kusema kuwa ni mzuri na kama Simba wakimpata anaweza kuwasaidia kwa kuwa anajua sana soka, lakini hawakuwa na mipango naye kwa wakati huo,” kilisema chanzo kimoja cha uhakika kutoka Simba.

Ukonde mwenye uwezo wa kutumia vyema guu lake la kushoto, rekodi zinaonyesha msimu huu kwenye Kombe la Shirikisho akiwa amecheza mechi mbili moja akicheza kwa dakika tisini na dakika 34 kwa mchezo wake wa pili.

Lakini katika Ligi Kuu ya Msumbiji, kiungo huyo amehusika katika mechi nne wakishinda moja, mbili wakiwa wametoka sare na moja wakiwa wamepoteza.

Kwa mujibu wa taarifa za kuaminika kutoka ndani ya Yanga zinasema kuwa kufika mapema kwa kiungo ilikuwa ni kwa lengo la kutaka kumtumia kwenye michuano ya Kombe la Kagame kabla ya uongozi kubadili maamuzi yao.

“Ni kweli Jimmy yupo nchini na jambo ambalo limepelekea awahi kufika ni kwa sababu ya Kagame maana aliambiwa juu ya hii michuano, akaridhia kucheza ndiyo maana amekuja mapema ila uongozi ukawa umebadili maamuzi kwa kuondoa jina lake.

“Lakini si peke yake hata Makambo alipigiwa simu akawa amekubali ila uongozi ulichoamua kwa Jimmy ndiyo ulichoamua kwa Makambo,” alisema mtoa taarifa.

Katika hatua nyingine, Yanga imemsajili aliyekuwa beki wa Mbeya City na Singida United, Roland Msonjo katika kuhakikisha wanaboresha safu yao ya ulinzi kwenye msimu ujao wa Ligi Kuu Bara.

IBRAHIM MUSSA, Dar es Salaam

Leave a Comment