
KATIKA kuelekea mchezo wa leo Jumamosi wa Ligi Kuu Bara dhidi ya KMC, wachezaji wawili wa Yanga wanatarajiwa kupangua kikosi hicho ambacho kinaongoza katika msimamo. Yanga inaongoza katika msimamo wa ligi ikiwa na pointi 45 huku Simba ikifuatia 37, Azam FC 28 na Namungo FC 25, sawa na Mbeya City.
Katika mchezo huo utakaopigwa leo Jumamosi saa moja kamili usiku kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam, Yanga wataingia wakiwa vifua mbele baada ya kuwafunga KMC mabao 2-0 katika mchezo wa mzunguko wa kwanza wa ligi.
Mmoja wa mabosi wa Benchi la Ufundi la timu hiyo, ameliambia Championi Ijumaa kuwa beki kiraka Shomari Kibwana huenda akarejea kucheza nafasi ya beki wa kushoto ambayo alikuwa akiicheza tangu kuanza kwa msimu huu katika mchezo dhidi ya KMC.
Bosi huyo alisema kuwa wakati Kibwana akirejea kucheza beki wa kushoto, Farid Mussa ambaye alikuwa anacheza namba tatu, sasa atarejea kwenye nafasi yake ya namba 7. Nafasi ya namba 7 imekuwa ikichezwa na Mkongomani Jesus Moloko aliyeanza mazoezi mepesi ya gym baada ya kupata nafuu ya majeraha ya goti.
Akirejea atakutana na ushindani mkubwa wa namba. Aliongeza kuwa kurejea kwa Kibwana kumefanya mabadiliko hayo mawili katika kikosi cha Kocha Mkuu Mtunisia, Nasreddine Nabi katika kuelekea mchezo huo mgumu.
“Kama unakumbuka vizuri Farid alikuwa akichezeshwa namba tatu kama beki wa pembeni ni baada ya wachezaji waliokuwa wakicheza nafasi hiyo kupata majeraha na kocha Nabi alimbadilisha kucheza beki baada ya kumuona anaimudu.
“Hivyo katika kuelekea mchezo dhidi ya Azam, Nabi atamhamisha Farid kwa kumsogeza kucheza juu namba saba ambayo ndiyo nafasi yake huku Kibwana akirejeshwa katika nafasi yake.
“Kocha ameshaanza kuwaandaa wachezaji hao mazoezini tangu timu hiyo iliporejea kambini juzi Jumatatu kujiandaa na mchezo huo muhimu kwetu kupata pointi tatu.
“Tunafahamu KMC wakikutana na Yanga wanabadilika kucheza kwa kupania, lakini licha ya kupania kwao tutahakikisha tunawafunga kwani siyo hao pekee, zipo timu nyingi zikikutana na sisi zinatupania,” alisema bosi huyo.
Akizungumzia hilo, Nabi alisema: “Ninafurahia kuona wachezaji wangu waliokuwa majeruhi wakipona na kurejea kuipambania timu yao, hivyo katika mchezo ujao dhidi ya KMC tutakuwa na mabadiliko machache ya wachezaji katika baadhi ya nafasi.
“Kibwana (Shomari), Chico (Ushindi), Bryson (David) na Yassin (Mustapha) wote wamepona na wapo fiti tayari kucheza mchezo huo dhidi ya KMC.”
Wilbert Molandi, Dar es Salaam