
KIUNGO wa zamani wa Simba Mbrazili, Gerson Fraga Vieira amewagawa mabosi wa timu hiyo waliokuwa kwenye mipango ya kumrudisha kiungo huyo.
Simba inataka kumsajili Fraga kwa ajili ya kuimarisha safu ya kiungo baada ya kuonekana kuikosa saini ya kiungo Mganda, Khalid Aucho aambaye tayari amemwaga wino Yanga.
Tayari zipo tetesi za Fraga kuwasiliana na uongozi wa Simba akiomba kurejea tena katika klabu hiyo baada ya kuwahakikishia yupo fiti. Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumatatu, wapo viongozi wanaomtaka na wasiomtaka katika usajili wa msimu ujao.
Mtoa taarifa huyo alisema kuwa viongozi wasiomtaka wenyewe wana hofu ya majeraha na wengine ukubwa wa mshahara. “Simba wapo katika mipango ya kumsajili kiungo mmoja wapo kati ya Fraga au Aucho waliokuwa kwenye mazungumzo atakayekuja kusaidiana na Lwanga (Tadeo).
“Fraga yeye mwenyewe amewasiliana na viongozi akiomba kurejea Simba baada ya kupona majeraha yake ya goti.
“Lakini wapo baadhi ya viongozi wanaomtaka na wasiomtaka, hivyo bado wanavutana katika kukamilisha usajili wake. Ofisa Habari wa timu hiyo, Ezekiel Kamwaga juzi alizungumzia usajili kwa kusema kuwa “Kila usajili unaokamilika unawekwa wazi kwa kuutambulisha, hivyo uongozi upo bize na usajili hivi sasa.”
WILBERT MOLANDI, Dar es Salaam