×

Idris na Wenzake Waachiwa Huru

HATIMAYE Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam imemfutia kesi na kumwachia huru msanii wa Bongo Movies na comedy, Idris Sultani pamoja na wenzake wawili kufuatia Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Tanzania (DPP) kuieleza mahakama hiyo kuwa hana nia ya kuendelea na kesi hiyo leo Jumanne, Agosti 17, 2021.

 

Idris na wenzake walikuwa wakikabiliwa na shtaka moja la kuchapisha maudhui mtandaoni bila kuwa na kibali kutoka Mamlaka ya MAwasiliano Tanzania (TCRA). Washtakiwa hao wamefutiwa mashtaka chini ya kifungu namba 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ( CPA) Sura ya 20, iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2019.

 

Maamuzi hayo yametajwa na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Yusto Ruboroga, baada ya upande wa mashtaka kuwasilisha hati mahakamani hapo ya kutokuwa na nia ya kuendelea na mashtaka hayo huku Wakili wa Serikali, Neema Mosha, akisema kesi hiyo imeitwa kwa ajili ya kusikiliza Ushahidi, lakini DPP, hana nia ya kuendelea na shauri hilo.

 

Baada ya Wakili Mosha kueleza hayo, Hakimu Ruboroga, alisema kupitia kifungu tajwa hapo juu, mahakama imewafutia mashtaka washtakiwa wote na kuwaachia huru kuanzia leo.

 

Watuhumiwa wengine katika kesi hiyo walikuwa ni Isihaka Mwinyimvua (22) ambaye ni mkazi wa Gongolamboto na Doctor Ulimwengu (28) ambaye ni mkazi wa Mbezi Beach (wote jijini Dar). Washtakiwa hao walikuwa akidaiwa kuchapisha maudhui katika mtandao wa Locomotion TV bila ya kuwa na kibali kutoka TCRA kinyume cha sheria ya Mawasiliano ya Mwaka 2016.

Leave a Comment