
Rais mataafu wa Marekani, Donald Trump amemtaka Rais wa nchi hiyo, Joe Biden ajiuzulu akimtuhumu kusababisha Wanamgambo wa Kundi la Taliban kupata nafasi ya kutawala Miji mbalimbali ya Afghanistan ikiwemo Mji Mkuu wa Kabul, hii ikiwa ni baada ya uamuzi wake kuliondoa Jeshi la Marekani nchini humo lililokaa kwa miaka takribani 20.
“Ni wakati umefika sasa kwa Joe Biden kujiuzulu kwa kile alichokisababisha kwa Watu wa Afghanistan na wala haitokuwa jambo kubwa maana hakuteuliwa kihalali tangu mwanzo, Biden ameshindwa pia kuidhibiti Corona, kupambana na masuala ya Uchumi na Wahamiaji” amesema Trump.
Rais wa Afghanistan Ashraf Ghani ameikimbia Nchi yake ya Afghanistan juzi baada ya Wanamgambo wa Taliban kuuzingira mji mkuu wa Kabul.
Hata hivyo Rais Biden ametetea uamuzi wake wa kuondoa majeshi yake nchini Afghanistan licha ya nchi hiyo kutekwa na Taliban.
Biden amesema ameidhinisha vikosi zaidi vya Wanajeshi 5,000 wa Marekani viende Kabul, kusaidia ulinzi wa ubalozi wa Marekani na kuwaondoa wafanyakazi wake kutoka Taifa hilo linaloelekea kuangukia mikononi mwa Wanamgambo wa Taliban.