
MWANAMAMA wa Bongo Movies, Irene Pancras Uwoya au Mama Krish anakuambia ni mwendo wa bata juu ya bata kwani baada ya kufanya kufuru za kufa mtu kule Dubai, sasa amehamishia bata visiwani Zanzibar, lakini jeuri hiyo inatajwa kutoka kwa kigogo mmoja mzito nchini Kenya.
Akiwa Dubai, Uwoya aliliambia gazeti pacha la hili la IJUMAA kuwa, aliteketeza zaidi ya milioni 80 za Kibongo kwa ajili ya kulipia hoteli ya nyota tano aliyofikia na mwanawe, Krish Ndikumana na watu wengine wawili alioambatana nao.Uwoya alitumia takriban wiki tatu kula bata za kufuru Dubai huku akiwarusha roho mastaa wengine.
Akiwa huko, usafiri wake wa hapa na pale ulikuwa ni gari za kifahari kama Rolls Royce ambalo alikuwa akitumia kama teksi na wakati mwingine alikuwa akitumia usafiri wa helikopta

ATUA BONGO, NI ZAMU YA ZANZIBAR
Mara tu baada ya kutua Bongo wikiendi iliyopita, Uwoya hakulala Tanzania Bara kwani alikwea tena pipa na kutua Zanzibar ambako bata linaendelea.
ATUMIA RANGE ROVER KAMA TEKSI
Akiwa Zanzibar, Uwoya anatumia usafiri wa gari la kifahari, lakini huko siyo Rolls Royce, bali ni Range Rover Sport kama lile alilonunua mrembo wa Bongo Fleva, Faustina Charles almaarufu Nandy ambalo limemgharimu zaidi ya shilingi milioni 100 za Kitanzania.Kama kawaida, bata hilo la Uwoya limeendelea kuzua maswali kwani ana muda mrefu haonekani akiigiza au kufanya biashara kwani alishafunga hata ile baa yake ya Last Minute ya Sinza-Mori jijini Dar.

URITHI WA KRISH?
Wapo baadhi ya watu wanaodai kwamba, Uwoya anatanua kutokana na urithi wa mwanawe, Krish alioachiwa na baba yake, marehemu Ndikumana.Itakumbukwa kwamba, Ndikumana alikuwa msakata kabumbu wa kimataifa ambaye alicheza soka la kulipwa hadi Ulaya hivyo kuwa na mali nyingi.
KIGOGO KENYA ATAJWA
Lakini kubwa kuliko, kumekuwa na tetesi nyingine kwamba, bata la Uwoya linasababishwa na kigogo mmoja mkubwa katika Serikali ya Kenya.Inadaiwa kwamba, kigogo huyo ambaye kwa sasa tunamhifadhi, lakini tutamtaja hivi karibuni ndiye ambaye amekuwa akimpa jeuri yote Uwoya.

MWENYEWE AFUNGUKA
Katika mahojiano maalum (exclusive interview) na gazeti bora la mastaa ndani na nje ya Bongo la IJUMAA wiki mbili zilizopita juu ya ulaji wake bata hadi kuku wananuna, Uwoya alisema kuwa, mara nyingi yeye hapendi kujionesha kwenye mitandao ametumia kiasi gani kwenye matanuzi yake.
Hata hivyo, alisema kuwa, kwa kila kitu kipo kwenye mitandao ya kijamii ni vyema watu wakaangalia hoteli hiyo ambayo amefikia na watu wake hao na wakaangalia bei zake za kulala kwa siku moja ili wapate majibu kuliko kuendelea kusemasema vitu ambavyo hawana details (maelezo ya uhakika) navyo.

“Unajua maisha ya kuweka wazi kila kitu kuna wengine watashindwa kupumua kabisa, lakini kwa kuwa kila kitu kipo wazi kwenye mitandao na mimi nataka mtu mwenyewe aone kwa macho yake na siyo kuambiwa.“Hii ndiyo maana na mimi naendelea na maisha yangu na kujipa furaha mwenyewe wala sisubiri kupewa na mtu,” alisema Uwoya ambaye amedumu kwenye ustaa kwa zaidi ya miaka 15.
Akiendelea kuzungumza na IJUMAA, Uwoya alisisitiza kuwa ni vyema mtu kuwa na furaha ndani ya moyo kwa sababu kila mtu ana jukumu la kutafuta furaha yake bila kukumbushwa.
Alisema kuwa, katika mazingira kama hayo ameamua kujipa furaha yeye na mwanawe, Krish kwa sababu ndivyo inavyotakiwa watu waishi kila siku na si kweli kwamba anafanya hivyo kuwaumiza watu wengine.
“Mimi ni mtu ambaye ninajali sana furaha yangu bila kujali mtu atasema nini na ndiyo maana watu wanaweza kusema ninakula bata tu, lakini hiyo ndiyo maana ya furaha kwa sababu ndicho kitu ninachokipenda kila wakati.

“Mimi ninajali sana nafsi yangu inataka nini siku zote,” anasema Uwoya ambaye hivi karibuni alitangaza kuokoka.Hata hivyo, miongoni mwa maswali ambayo Uwoya amekuwa mgumu kuyajibu ni pamoja na jeuri hiyo ya pesa anaipata wapi huku akisisitiza kwamba, ili mtu ale bata si lazima ategemee kupata jeuri kutoka kwa mtu kwa kuwa ana uwezo wa kutafuta pesa zake mwenyewe.“
Unajua kutumia pesa, siyo kwamba mtu una pesa sana, maana inawezekana kuna watu wako wa karibu wamekusaidia kwenye hilo. Naomba watu waache kumuangalia mtu kwa mtazamo hasi wa nje, wajifunze hilo,” alisema Uwoya ambaye mbali na marehemu Ndikumana, pia aliwahi kuolewa na msanii wa Bongo Fleva, Abdulaziz Chande ‘Dogo Janja’.