
MKONGWE wa Manchester United, Gary Neville amefunguka kuwa timu hiyo inatakiwa kujipanga kwani msimu ujao, Paul Pogba ataondoka na kujiunga na Real Madrid au PSG.
Pogba wikiendi iliyopita alifanya vizuri na kuibeba Man United kwenye mchezo wa ufunguzi wa Premier League akitoa pasi nne za mabao.
Kiungo huyo amekuwa akihusishwa kujiunga na PSG msimu huu kipindi cha majira ya joto akiwa amesalia na mwaka tu ndani ya United.
Neville anaamini kuwa huu ni msimu wa mwisho wa Pogba ndani ya Man United hivyo wanatakiwa kujipanga.
“Man United wanatakiwa kujua kuwa Pogba ataondoka msimu ujao. Naona atafanya vizuri msimu huu hapa, lakini sina hakika kama malengo yake ni kubaki hapa.“
Malengo yake ni kucheza sehemu nyingine sio hapa nadhani kwa sasa anafikiria pakwenda kama ni Real Madrid au PSG.“Kwa hiyo, Man United wanatakiwa kujiandaa kwa sasa kujua ni kitu gani kitafuata baada ya hapo.”