×

Waziri Achukua Pesa za Umma Kufanya Honeymoon, Yamkuta

Mamlaka ya kupambana na rushwa nchini Malawi, ACB imemkamata aliyewahi kuwa waziri wa maji na maendeleo ya umwagiliaji nchini humo, Charles Mchacha kwa madai ya kuilazimisha Bodi ya Maji ya Lilongwe (LWB), kumlipia fedha za fungate, vyakula na vinywaji kinyume cha sheria.

 

Mchacha anatajwa kushirikiana na aliyekuwa katibu mkuu wa wizara hiyo, Dkt. Henrie Njoloma na kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Lilongwe, Moses Mwenye ambapo waliidhinisha malipo ya fungate lake katika Hoteli ya Kifahari ya Ryalls iliyopo jijini Blantyre Serikali kiasi cha Kwacha 539,000 (Tsh 1,538,667).

 

Mwanasiasa huyo ambaye kwa sasa ni Mbunge wa Jimbo la Thyolo Magharibi kwa tiketi ya Chama cha Democratic Progressive Party (DPP) anatuhumiwa kwa makosa ya matumizi mabaya ya madaraka na ubadhirifu, ambapo fedha alizozitumia, zilikuwa ni malipo ya ankara za maji za wananchi.

 

Taarifa iliyotolewa na Afisa Habari wa ACB, Egrita Ndala inazidi kueleza kuwa mshtakiwa wa pili, Njoloma na mtuhumiwa wa tatu,  ambaye alikuwa Mkurugenzi wa Bodi hiyo ya maji, walimsaidia Mchacha kutimiza ufisadi huo kwa kuandaa hati za malipo, wakati wakijua kwamba ni kinyume cha sheria.

 

Watatu hao walikamatwa Alhamisi kufuatia uchunguzi maalum wa Mamlaka ya Kuzuia Rushwa nchini humo (ACB). Mamlaka hiyo imesema ilipokea malalamiko kwamba Bodi ya Maji imelipia Honeymoon ya Mchacha.

 

Mchacha, ambaye ni mbunge wa Jimbo la Thyolo Magharibi anatuhumiwa kutumia vibaya madaraka yake kwa kumshinikiza moja kwa moja Njoloma kulipia gharama za malazi na vyakula katika hoteli hiyo kwa kutumia pesa za umma kinyume cha sheria.

 

Inazidi kuelezwa kwamba tuhuma dhidi ya Mchacha ziliwasilishwa kwa mamlaka ya kupambana na rushwa Agosti 24, 2020 na baada ya kuzifanyia kazi kwa takribani mwaka mzima, hatimaye Agosti 26, 2021 watuhumiwa wote watatu walikamatwa.

 

Kwa mujibu wa mamlaka hiyo ya kupambana na rushwa, watatu hao watapandishwa kizimbani kujibu tuhuma za matumizi mabaya ya ofisi, rushwa, uzembe na ubadhirifu.

 

Hakimu Mkazi Mkuu, Patrick Chirwa jana aliruhusu dhamana kwa washtakiwa hao yenye masharti matatu ikiwemo kuweka bondi ya Kwacha 500,000 (Tsh 1,427,579) kila mmoja, kusalimisha nyaraka zao za kusafiria.

 

Mahakama imemwamuru Mchacha aliyekuwa waziri wakati wa utawala wa Rais wa zamani, Peter Mutharika kuripoti katika Ofisi za Mamlaka ya Kupambana na Rushwa iliyopo Blantyre na wale walioko Lilongwe waripoti katika ofisi za mamlaka hiyo zilizopo Lilongwe kila Ijumaa na kesi hiyo imeahirishwa mpaka Septemba 1, mwaka huu itakapoendelea tena.

Leave a Comment