×

Rigwaride Ra Afande – 6

ILIPOISHIA RISASI JUMATANO:
“Kama upo sawa hebu fungua mlango basi,” ilisema sauti nyingine lakini nayo niliikumbuka ni ya yule afande wa pili aliyenikatia nusu laki.

Nilijua kimenuka, msichana naumbuka. Tena mbaya zaidi naumbukia kwa mtu niliyeamua kwenda naye bureee! Kwa kumwonea huruma…
“Fungua bwana…inasemekana uko na kale kabinti…”
TAMBAA NAYO MWENYEWE…

Nilimwona afande Mwira anatetemeka, lakini hakunishinda mimi. Nilitetemeka zaidi kwani nilianza kuhisi hali ya kupoteza fahamu kutokana na kuzomewa kwa kitendo changu cha kuwanyang’anya wanaume watatu kwenye nyumba moja na kwa siku moja, tena muda huohuo.

Nilimtaka afande Mwira asingue kwani kufanya hivyo kungenileta balaa zaidi kuliko kutofungua…
“Na leo atakula jeuri yake,” yule mbaba wa mwanzo alisema ndiyo nikazidi kuchanganyikiwa zaidi, nikaogopa sana.

Ilifika mahali nikahisi nataka kulia, niliulaumu sana moyo wangu kwa kitendo kile.
Sasa wale maafande wakawa wanagonga mlango kwa nguvu huku wakitishia kuvunja kama yule afande niliyenaye hatafungua mlango mwenyewe.

“Kwani siwezi kupita kwenye hili dirisha?” nilimuuliza baada ya kuangalia dirisha na kugundua halina zile nondo zinazokatisha katikati ili mwizi asipite. Ni zile nyumba zilizojengwa zamani kidogo.

Cha ajabu yule afande chumbani badala ya kunijibu, akawa eti anataka tuendelee na zoezi letu la mechi ya kitandani. Nikamkatalia katakata na kutoka kitandani…

“Hivi wewe una ukali kweli? Yaani unaona kabisa unagongewa na wenzako tena wanaonekana wanajua kila kitu halafu bado unataka tuendelee!” nilimsema nikiwa napanda dirisha, akanisaidia kutoka kwa kunisukuma, nikaangua upande wa pili…tii!
Kusema ukweli niliumia, hata niliposimama ili nitembee nilijikuta nachechemea.

Nikachechemea mpaka nyumbani ambapo mama aliponiona nachechemea akataka kujua kisa…
“Nimeumia mama…”
“Umeumia na nini?”
“Nilianguka kwenye mtaro mama.”

“Kwanza unatoka wapi?”
“Nilikwenda sokoni mama…”
“Kununua nini na nani amekutuma?”
“Vitu vyangu…”

“Viko wapi?”
Niliangalia chini kwa aibu maana maswali ya mama yalikuwa ya msingi…
“Si nakuuliza wewe!”

“Nisamehe mama,” nilisema nikiwa naangalia chini kwa aibu…
“Kwanza hutoki kwa mwanaume wewe?” mama alinipiga swali jingine gumu sana. Nilitetemeka, moyoni nikasema…
“Si mwanaume mama, natoka kwa wanaume watatu, hapa nimechoka ile mbaya.”
“Si nakuuliza wewe.”

“Ndiyo mama…”
“Sasa..?”
“Sitoki huko mama…”
“Twende chumbani kwako.”

Jamani, mama yangu namfahamu vizuri sana, aliposema twende chumbani kwangu nilijua anataka akanipekue. Sasa unadhani ingekuaje?! Ningekubali kwenda? Wee!
“Mama nisamehe, tusiende chumbani.”

“Basi niambie ukweli.”
Nilishindwa kumwambia ukweli mama. Hata ungekuwa wewe ungemwambiaje!
“Leo humu ndani huingii mpaka useme unatokea wapi?”
“Mama natoka kwa rafiki yangu.”
“Wapi?”
“Temeke Mwisho.”

“Twende sasa hivi tukamuulize kama kweli wewe ulikwenda kwake. Usimpigie simu wala usimtumie meseji,” alisema mama. Alinipa mawazo mengine tena, nikaona hakuna haja, ni kulisanua tu.

“Mama nilikwenda kwa mwanaume kweli,” nilimwambia mama huku nikimwangalia kwa macho ya umakini sana ili asije akanivaa na kunipiga.
“Mwanaume gani?”
“Simjui mama…”

“Ha! We mtoto…mwanaume humjui na unakwenda kwake? Twende sasa hivi ukanioneshe hiyo nyumba uliyoingia,” alisema mama akinishika mkono.
Kweli, mama hakuwa na mchezo wala utani, tulianza safari. Mama yangu mimi ni mkali sana hivyo sikuweza kumkatalia hata kidogo.

Tulikata mtaa, tukatokezea kwa mbele, tukaingia barabara kuu, tukavuka, tukatokea kwenye mtaro, tukauruka.

Sasa watu wakawa wanatuangalia. Wapo waliosema napelekwa kuozeshwa kwa nguvu, wapo waliosema nakwenda kukeketwa, wengine walisema napelekwa hospitali kutolewa mimba maana ni mitaa ya hospitali.

Nilifikiria namna ya kumpotosha mama, kwamba badala ya kumpeleka pale kwa jina afande Mwira nitafute nyumba yoyote yenye kufuli niseme ni hapo, lakini mwenyewe katoka…

“Bado hatujafika?” mama aliniuliza kwa ukali. Aibu hana wala kuniwazia mimi kwamba naaibika, wala!

“Ni pale mama, tumefika,” nilimwambia nikimwonesha nyumba nyingine nikijua mlango umefungwa lakini kumbe wenyewe walikuwepo maana ile tunakaribia tu, wakatoka wanawake watatu.

“Ndiyo pale wanapotoka wale wanawake?” aliniuliza mama.
“Hapana, kwa nyuma.”
Na kweli, kwa nyuma ndiyo nyumba ya akina afande Mwira ilipo, tukafika sasa…
Je, nini kiliendelea hapo? Usikose kusoma kweli Risasi Jumatano ijayo.

Leave a Comment