
RAIS wa guinea, Alfa Conde, mwenye umri wa miaka 83, alizuiliwa na wanajeshi wa kikosi maalum (GFS) jana Septemba 5, 2021 katika Ikulu ya nchi hiyo ikiwa ni saa kadhaa baada ya kuripotiwa kwa ufyatulianaji wa risasi karibu na makazi ya Rais huko Conakry.
Kamanda wa GFS, Kanali Mahamady Doumbouya alithibitisha kuchukua serikali kupitia Runinga ya serikali na kuahidi kusimamia mabadiliko ya serikali kwa njia ya amani.
“Ubinafsishaji wa maisha ya kisiasa umekwisha. Tutaweka mpango wa mpito ulio wazi na unaojumuisha watu wote. Tutaweka mfumo ambao [sasa] haupo,” Doumbouya alisema wakati akiwa amezungukwa na maafisa wa GFS wenye silaha waliojifunika bendera ya Guinea.
Kanali Doumbouya, ambaye anasemekana alipata mafunzo ya kijeshi nchini Ufaransa, anaonekana kuwa katika uongozi wa kikosi cha jeshi kilichochukua madaraka nchini Guinea kwa jina la National Committee for Rally and Development (CNRD).
“Hali ya kijamii, kisiasa na kiuchumi ya nchi, kutofanya kazi kwa taasisi za jamhuri, udanganyifu wa mfumo wa haki, ukiukaji wa haki za raia, kutokuheshimu kanuni za kidemokrasia, siasa nyingi katika utumishi wa umma, usimamizi mbaya wa kifedha, umasikini na ufisadi umesababisha jeshi la jamhuri kuchukua majukumu yake kwa watu wa Guinea.
“Lazima tusaidie watu wa Guinea kutoka katika hali hii kwa sababu tunaihitaji. Tunamsihi kila mtu akae katika kambi yao na aendelee na shughuli zao za za kawaida ambazo ni pamoja na kulinda mipaka.
“Lengo letu ni kuhakikisha kuwa watu wa Guinea wana umoja na wanapata faida zote za nchi. Hatujaja kufanya mzaha na serikali. Tutajifunza kutokana na makosa yote ambayo tumefanya na watu wote wa Guinea,” alisema Doumbouya.
Kuhusu Kanali Doumbouya
Mengi hayajulikana sana juu ya maisha ya utotoni ya Doumbouya, isipokuwa kwamba yeye ni kutoka kabila la Malinke kama Rais Conde na anatoka Mkoa wa Mashariki wa Kankan wa Guinea. Alikuwa huko Forecariah, magharibi mwa Guinea, ambapo alihudumu chini ya ofisi ya uchunguzi wa eneo (DST) na huduma za ujasusi.
Ana uzoefu wa miaka 15 wa kijeshi ambayo ni pamoja na misheni nchini Afghanistan, Cote d’Ivoire, Djibouti, Jamhuri ya Afrika ya Kati na ulinzi wa watu mashuhuri Israeli, Cyprus, Uingereza na Guinea.
Kanali huyo anasemekana “amekamilisha vyema” mafunzo ya wataalam wa ulinzi wa kiutendaji katika Chuo cha Usalama cha Kimataifa huko Israeli, kozi ya mafunzo ya makamanda wa shule katika Shule ya mafunzo ya kijeshi Senegal, mafunzo ya afisa msimamizi Chuo cha staff College Libreville (EEML) cha Gabon na Chuo cha Vita huko Paris.
Alihudumu kama mwanajeshi wa kigeni yaani ‘legionnaire‘ katika Jeshi la Ufaransa hadi 2018 wakati Conde alipomtaka arudi Guinea kuongoza GFS, iliyoanzishwa mwaka huo.
Maisha yake
Tangu 2018, kumekuwa na ripoti kadhaa kwenye vyombo vya habari vya Guinea zikitilia shaka sifa za Doumbouya. Mnamo Oktoba 2018, Le Guepard aliwaonya watu wa Guinea dhidi ya “kuanguka chini ya ulimi mtamu wa mtu atakayewanyonga siku za usoni”.
Mnamo Agosti 2021, Friaguinee lilidai kwamba Dombouya alinyimwa uraia wa Ufaransa kwa sababu “mwenendo wake ulionekana kuwa kinyume na maadili na kanuni” za jeshi la Ufaransa. Ilihoji pia chanzo cha utajiri wa kanali huyo.
Wakati ikiripoti kuhusu mali kadhaa zinazodaiwa kuwa ni za kanali Doumbouya, Friaguinee iliuliza: “Afisa huyu, ambaye anapokea mshahara wa kila mwezi wa chini ya faranga milioni tano [$ 500], anawezaje kujenga majengo haya yote?”
Mnamo Mei, Doumbouya alikuwa miongoni mwa maafisa 25 wa Guinea waliolengwa kwa vikwazo vya EU juu ya ukiukwaji wa haki za binadamu. Ni kufuatia uvumi wa kuzuiliwa kwa watu katika Camp Dubreka magharibi mwa Guinea lakini vikwazo hivyo vilifutwa haraka. Doumbouya pia anaonekana alikuwa akipinga wizara ya ulinzi kusimamia kikosi cha GFS.