×

Gomes Awapa Mtihani Mastaa Wake


SIRI imefichuka kuwa kocha Mkuu wa Simba, Didier Gomes ndiye ameutaka uongozi wa timu hiyo kumtafutia timu kubwa hapa Afrika ya kucheza nao katika siku ya tamasha la ‘Simba Day’ ili kupima ni namna gani nyota wa kikosi hicho wamepokea programu za mazoezi yake kabla ya msimu.

 

Simba inatarajia kufanya tamasha hilo la Simba Day, Septemba 19, mwaka huu katika Uwanja wa Mkapa Dar es Salaam, ambapo tayari uongozi wa klabu hiyo umeweka wazi unatarajia kualika timu kubwa ambayo imewahi kutwaa ubingwa wa Afrika kwa mara tatu na zaidi.

 

Simba inaendelea na kambi ya kujiwinda na msimu ujao ambapo kwa sasa kikosi hicho kipo kwenye awamu ya pili ya kambi yao inayofanyika Karatu Arusha.

 

Akizungumza na Championi Jumatatu, Kaimu Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga alisema: “Maandalizi ya tamasha la siku ya Simba ‘Simba Day’ ambayo mwaka huu itafanyika Septemba 19, yanaendelea vizuri, mpaka sasa tumesaliwa na takribani wiki mbili tu kufikia siku hiyo na tayari taratibu mbalimbali ikiwezo uuzaji wa tiketi unaendelea kufanyika.

 

“Pamoja na burudani nyingine ambazo zitakuwepo siku hiyo kama vile burudani ya muziki kutoka kwa wasanii wa ndani na nje ya nchi, lakini pia kama ambavyo tumeweka wazi kuwa tunatarajia kuwa na mchezo dhidi ya timu kubwa hapa Afrika ambayo ni mapendekezo ya kocha mkuu, Didier Gomes ambaye anataka kupima mapokeo ya programu za mazoezi alizowapatia wachezaji wake.”

JOEL THOMAS, Dar es Salaam

Leave a Comment