×

Gomes Bado Kidogo tu Simba

KOCHA Mkuu wa Simba, raia wa Ufaransa, Didier Gomes, amebakiza kazi ndogo tu kuhakikisha anakuwa na kikosi imara kabla ya kuanza kwa msimu wa 2021/22.

 

Gomes raia wa Ufaransa, katika muda uliobaki wa maandalizi yake, ana dakika tisini za kucheza mechi ya kirafiki akiwa kambini Arusha ambapo mchezo huo uliopigwa jana Jumanne dhidi ya Aigle Noir ya Burundi, kabla ya kurudi Dar kwa ajili ya Tamasha la Simba Day, Jumapili hii.

 

Katika Simba Day itakayofanyika Uwanja wa Mkapa, Dar, Simba inatarajiwa kucheza mechi nyingine ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya TP Mazembe ya DR Congo, kisha Septemba 25, mwaka huu uwanjani hapo itapambana na Yanga katika mechi ya Ngao ya Jamii, kufungua msimu wa 2021/22.

 

Akizungumza na Spoti Xtra, Mratibu wa Simba, Abbas Ally, alisema wakiwa kambini Arusha, kocha huyo aliomba michezo mitatu ya kirafiki ambapo tayari wamecheza miwili dhidi ya Coastal Union na Fountaine Gate, bado mmoja.

 

Aliongeza kuwa, mchezo huo wa mwisho ndiyo utampa mwanga wa kujua nani aingie katika kikosi chake cha kwanza kati ya baadhi ya nyota wapya waliosajiliwa ambao ni Peter Banda, Ousmane Sakho na Sadio Kanoute.

 

“Baada ya kucheza michezo miwili ya kirafiki dhidi ya Coastal Union na Fountaine Gate huku kambini kwetu Arusha, timu itacheza mchezo mwingine wa mwisho kabla ya wiki hii kurejea Dar kwa ajili ya Simba Day.

 

“Michezo hiyo aliiomba kocha kwa ajili ya kuangalia ubora wa kikosi chake, upungufu na kupata kikosi cha kwanza atakachokitumia Simba Day.

 

“Mchezo huo tutaucheza ndani ya siku hizi mbili, hivyo tunaamini muda huu tuliokaa kambini umetosha kabisa kocha kufanya maandalizi ya kutosha,” alisema Ally.

Mechi ya kwanza dhidi ya Coastal, matokeo yalikuwa 0-0 na dhidi ya Fountain Gate, Simba ilishinda 1-0.

WILBERT MOLANDI, Dar

Leave a Comment