
YANGA imepanga kutumia ndege ya kukodi kuwafuata wapinzani wao, Rivers United ya Nigeria kwa ajili ya kuwahi mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Simba utakaochezwa Septemba 25, mwaka huu Uwanja wa Mkapa, Dar.
Jumapili hii, Yanga itarudiana na Rivers, huko Port Harcourt, Nigeria, ukiwa ni mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya awali baada ya mchezo wa kwanza uliochezwa Jumapili, Yanga kufungwa bao 1-0.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Spoti Xtra, Yanga imepanga kuelekea Nigeria kesho Alhamisi wakiwa na msafara wa wachezaji 28 na viongozi kumi.
Mtoa taarifa huyo alisema msafara huo utaondoka kwa ndege ya kukodi kwa lengo la kufika mapema na kuwahi kurudi ili kujiandaa na mchezo wa Ngao ya Jamii.
Aliongeza kuwa, michezo hiyo miwili ina umuhimu mkubwa kwao, hivyo ni lazima wafanye maandalizi ya kutosha kuhakikisha wanapata matokeo mazuri.
“Kikosi kinatarajiwa kuondoka mapema jijini Dar es Salaam kuelekea Nigeria kwa ajili ya mchezo wa marudiano wa hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Rivers United.
“Katika kikao tulichokaa, viongozi wamekubaliana msafara wa timu utaondoka kwa ndege maalum ya kukodi ili kuhakikisha timu inafika mapema na pia inarejea haraka kujiandaa na mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Simba.
“Tunachukua usafiri wa kukodi kwa hofu ya kuwachosha wachezaji wetu ambao wana majukumu mazito mawili ndani ya siku chache,” alisema mtoa taarifa.
Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela, alipotafutwa kuzungumzia hilo, alisema: “Ratiba inatubana, tuna michezo migumu ambayo yote muhimu dhidi ya Rivers na Simba.
“Hivyo ni lazima tuchukue tahadhari za haraka kwa hofu ya kuwachosha wachezaji wetu kwa kutumia usafiri binafsi wa ndege utakaotupeleka Nigeria na kuturudisha nyumbani kwa ajili ya kuendelea na maandalizi ya mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Simba.
“Bado tuna nafasi ya kusonga mbele katika michuano hii mikubwa Afrika, kama wao wametufunga nyumbani, sisi pia tuna nafasi ya kuwafunga kwao, Wanayanga waondoe hofu, tunakwenda kupambana Nigeria.”
WILBERT MOLANDI, Dar