×

Wapiga kura wasuasua Handeni na Arusha Mjini leo

ar 2
Mkazi wa Arusha Mjini akipiga kura kumchagua mbunge wake leo.

UCHAGUZI wa Ubunge kwa majimbo ya Handeni na Arusha Mjini uliopangwa kufanyika Desemba 13, mwaka huu, umefanyika salama baada ya kuahirishwa Oktoba 25, mwaka huu, huku idadi ya wapiga kura ikionekana kuwa ndogo tofauti na chaguzi nyingine.

Wananchi wa majimbo hayo ya Handeni na Arusha walianza kupiga kura asubuhi ya leo Desemba 13, mwaka huu, kuwachagua wabunge hao ambao watawawakilisha katika kipindi cha miaka mitano.

Marudio ya uchaguzi huo katika Jimbo la Arusha mjini umefanyika kufuatia kifo cha aliyekuwa Mgombea wa Chama Cha ACT Wazalendo, Estomih Malla, aliyefariki siku chache kabla ya kufanyika kwa uchaguzi.

Wapiga kura walioandikishwa katika Daftari la wapiga kura katika Jimbo la Arusha mjini ni 317,814 huku taswira ya awali ikionyesha idadi ndogo ya wapiga kura waliojitokeza kushiriki tendo hilo halali la kikatiba.

ar 3

Msimamizi wa uchaguzi katika Jimbo hilo, Juma Idd, amesema Kata ya Themi ilikuwa na Vituo vya kupigia kura 26 lakini kuanzia asubuhi hadi wanakaribia kufunga vituo idadi ndogo ya wapiga kura ndiyo iliyokuwa inatawala ikilinganishwa na idadi ya watu waliojiandikisha.

Aidha, wagombea wanaoshiriki katika uchaguzi huo ni pamoja na Godbless Lema (CHADEMA) anayejaribu kurudi tena baada ya kuongoza katika kipindi kilichopita.

“Tumejipanga vilivyo na ninaamini wananchi watanirudishia ubunge leo, ili mjifunze kuamini basi ngoja matokeo yatoke, itakuwa ni kumbukumbu kwenye maisha yetu kwamba Imani thabiti huwa inaleta matokeo mazuri” alieleza Lema.

Polisi na Uchaguzi
Baadhi ya Askari wa Jeshi la Polisi leo asubuhi walikuwa wameimarisha ulinzi wakati wa kufanyika kwa zoezi hilo.

Kwa upande wake mgombea wa (CCM), Philemon Mollel, ambaye amepiga kura katika Kituo cha Shule ya Sekondari Kimandolu ameiambia FikraPevu kwamba watu walijitokeza kwa kiasi kikubwa kwa ajili ya kupiga kura, hivyo anaamini kwamba atachaguliwa.

Naye Zuberi Mwinyi wa Chama Cha Wananchi (CUF), aliyepiga kura katika Kituo cha MCA, Daraja Mbili, amesema uchaguzi wa mwaka huu hautakuwa na tatizo na kuwa ushirikiano wa vyama vinavyoshiriki wameonekana kuimarisha amani ndani ya Jiji hilo.

ar 4

Mgombea pekee Mwanamke wa Chama Cha ACT Wazalendo, Navoi Mollel, amepiga kura katika Kituo cha Shule ya Msingi Burka kata ya Olasiti, amesema endapo itatokea ameshindwa, ataendelea kushirikiana na jamii inayomzunguka ili kutatua kero zinazowakabili wananchi.

Uchaguzi huo umefanyika katika Vituo 721 kwenye kata 25 za Jimbo la Arusha Mjini.

Hata hivyo, Jeshi la Polisi mkoani Arusha leo lilimshikilia Diwani wa Kata ya Ngarenaro (Chadema), Issaya Doita kwa tuhuma za kusababisha vurugu katika kituo cha kupigia kura.

Jimbo la Handeni Mjini

Wakati huo huo, wagombea watano kutoka vyama vya ADC, CCM, CHADEMA, CUF na TLP, wamesimama kugombea nafasi ya ubunge katika Jimbo la Handeni Mjini mkoani Tanga kufuatia kifo cha aliyekuwa mgombea wa Jimbo hilo marehemu Dk. Abdallah Kigoda, kilichotokea siku chache kabla ya uchaguzi Oktoba 25, 2015.

Katika Jimbo hilo, wapiga kura 38,597 walijiandikisha kupiga kura katika vituo 114, ambapo pamoja na idadi kubwa hiyo ya waliojiandikisha bado mwitikio sio mzuri katika uchaguzi huo.

Msimamizi wa Kituo cha Shule ya Msingi, Kwenjugo namba moja, Othumani Twalibu, amezungumzia baadhi ya changamoto hizo kuwa ni pamoja na daftari la wapiga kura kutokuwa na picha za wahusika.

Msimamizi Mkuu wa Uchaguzi huo mdogo katika jimbo hilo, Tweneth Haule, amesema idadi ya wagipga kura ilikuwa ndogo.

Hadi tunaenda hewani, baadhi ya vituo vya kupigia kura vilikuwa hazijakalimisha zoezi la kuhesabu matokeo.

CREDIT: FIKRA PEVU

Leave a Comment