
Ofisa wa juu katika Wizara ya Fedha na Mipango, Renatus Msangira (45) ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha kuwa aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya, hakupata ruhusa wala kibali kutoka nje ya kituo chake cha kazi Januari 22, 2021 na kwenda jijini Arusha.
Akitoa ushahidi leo Alhamisi Septemba 23, 2021 katika kesi la uhujumu inayomkabili Sabaya na wenzake sita, Msangira ambaye ni mkurugenzi msaidizi anayesimamia utawala katika wizara hiyo ameiambia mahakama kuwa Sabaya alipaswa kuwa na kibali kutoka Mkoa wa Kilimanjaro.
Msangira aliwahi kuwa Katibu Tawala Msaidizi mkoa wa Kilimanjaro na ofisi yake ndiyo ilikuwa ikihusika na vibali. Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Enock Mnkeni, Watson Mwahomange, John Aweyo, Sylvester Nyegu, Jackson Macha na Nathan Msuya.
Akiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Felix Kwetukia, shahidi huyo alidai kati ya Machi 2020 hadi Juni 2021 alikuwa Katibu Tawala Msaidizi mkoa wa Kilimanjaro na ofisi yake ndio ilikuwa ikihusika na vibali.
Shahidi huyo aliieleza mahakama kuwa kwa mujibu wa taratibu, Mkuu wa Wilaya anaweza kutoka nje ya wilaya yake kufanya majukumu kwa kibali cha msimamizi wake ambaye ni Mkuu wa Mkoa. Alisema kibali hicho hutolewa iwapo mkuu wa wilaya husika atakuwa nje ya kituo cha kazi kwa sababu yoyote ya msingi.
Aliendelea kudai kuwa mkuu wa wilaya anapokuwa nje ya kituo chake cha kazi na nje ya mkoa wake lazima awe na kibali cha maandishi kinachomruhusu kutekeleza alichoenda kufanya nje ya kituo chake.
Mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo Patricia Kisinda, shahidi huyo wa kwanza wa Jamhuri amesema mtumishi wa umma anapaswa kuheshimu taratibuza za utumishi. Katika kesi hiyo leo, upande wa Jamhuri uliongozwa na Mawakili Waandamizi Tarsila Gervas, Felix Kwetukia, Othmed Mtenga na Wakili wa Serikali Neema Mbwana.
Upande wa utetezi uliwakilishwa na mawakili Mosses Mahuna, Charles Abraham, Edmund Ngemela na Sylvester Kahunduka.
Shahidi huyo amesema majukumu ya mkuu wa wilaya yameainishwa katika hati ya uteuzi ambayo mkuu wa wilaya hupewa baada ya kuteuliwa na Rais ambapo jukumu kubwa huwa ni kusimamia shughuli za ulinzi na usalama katika wilaya yake.
Lingine ni kusimamia shughuli za maendeleo na uhamasishaji maendeleo katika wilaya yake. Amesema ikitokea mkuu wa wilaya yuko nje yay a wilaya yake, anaweza kutekeleza majukumu kwa kibali cha msimamizi wake wa kazi ambaye ni Mkuu wa Mkoa.
Shahidi huyo amesema mkuu wa wilaya anapokua nje ya mkoa katika kutekeleza majukumu lazima kuwe na kibali cha maandishi kumruhusu kutekeleza hicho. Katika kesi hiyo Sabaya na wenzake wanashitakiwa kwa makosa matano likiwemo la kuongoza genge la uhalifu na utakatishaji fedha.
Washtakiwa wote wanadaiwa kujipatia Sh90 milioni kutoka kwa mfanyabiashara Fransis Mrosso huku wakijua kupokea fedha hizo ni zao la kosa la vitendo vya rushwa.
Katika kosa la pili, la tatu na la nne, Sabaya peke yake ameshitakiwa kwa makosa ya kujihusisha na rushwa ambapo anadaiwa kuchukua Sh90 milioni ikiwa ni matumizi mabaya ya ofisi akiwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Kilimanjaro. Kesi hiyo imeahirishwa hadi kesho ambapo shahidi wa pili atoa ushahidi wake.