×

Binti wa Miaka 21 Akutwa na Meno ya Tembo – Video


JESHI la Polisi Mkoa wa Kipolisi Rufiji limewakamata watu wawili (mwanamke mwenye umri wa miaka 21 na mwanaume mwenye umri wa miaka 40) wakiwa na nyara zinazodhaniwa kuwa ni meno ya tembo vipande 16 vyenye uzito wa kilo 25 ambapo thamani yake haijajulikana.

 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Rufiji, ACP Protas Mutayobya amesema tukio hilo lilitokea jana Alhamisi, Septemba 23, 2021 majira ya saa 1 jioni katika eneo Utunge, Kisemvule wilayani Mkuranga ambapo watuhumiwa hao walikuwa wamefunga vipande hivyo kwa mpita wa manati kwenye karatasi ya nailoni na ndani wameweka karatasi ya kawaida kisha kuviweka sebureni kwa ajili ya kuvisafirisha kwa ajili kuuza.

 

Aidha, Kamanda Mutayoba amesema katika oparesheni maalum inayoendelea kufanywa na jeshi hilo, mtu mmoja mwenye umri wa miaka 49 amekamatwa Septemba 16, 2021 akiwa na bangi kiasi cha kilo 150 iliyofungwa kwenye magunia sita pamoja na puli 14 katika eneo la Kimanzichana wilayani Mkuranga.

 

Ameeleza kuwa kiini cha matukio hayo ni kujipatia kipato kisicho halali hivyo vielelezo vyote vipo katika kituo cha polisi na wanaendelea kuwahoji watuhumiwa ili kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Leave a Comment