
MWINYI Zahera na Cedric Kaze ambao kwa nyakati tofauti waliifundisha Yanga kama makocha wakuu kabla ya sasa kurejea kikosini hapo kwa staili tofauti, wamekaa kikao na Kocha Mkuu raia wa Tunisia, Nasreddine Nabi na kumpa mbinu bora zaidi za kubeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara.
Zahera amerejeshwa Yanga kuwa Mkurugenzi wa Soka la Vijana, huku Kaze akirejea kama kocha msaidizi wa kikosi hicho.
Leo Jumatano, Yanga inashuka kwenye Uwanja wa Kaitaba, Kagera kuvaana na wenyeji wao, Kagera Sugar, ukiwa ni mchezo wa kwanza kwao wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2021/22.
Chanzo kutoka ndani ya Yanga, kimeliambia Spoti Xtra kwamba, siku chache kabla ya Nabi, kucheza na Simba, alipata fursa ya kukutana na Zahera na Kaze, ambao aliwaomba ushauri juu ya uzoefu wao ndani ya timu hiyo, ambapo kwa pamoja walimpa mbinu za kufanya vizuri.
“Naomba utambue tu kwamba, ushindi wetu wa Jumamosi dhidi ya Simba, umechangiwa kwa kiasi kikubwa sana na uwepo wa Zahera na Kaze, maana kabla ya mechi walipata fursa ya kumshauri Nabi, ambapo baadhi ya mambo muhimu aliyafanyia kazi.
“Ukiachilia mbali mechi hiyo, pia wamempa mbinu za kutwaa ubingwa kwa kumtaka asije akafanya kosa la kupumzisha wachezaji muhimu kwa ajili ya mchezo wa mbele yake, maana makosa kama hayo yaliwahi kuwagharimu.
“Pia kocha wamemwambia ugumu wa viwanja vya mikoani na kumtaka asiende bila tahadhari ya wachezaji wazoefu, maana wao ndiyo wanajua ugumu wa viwanja hivyo na kama atazingatia kutoruhusu kufungwa basi hadi mzumguko wa kwanza unaisha atakuwa amejihakikishia nafasi ya ubingwa,” kilisema chanzo hicho.
MUSA MATEJA, DAR