
KIONGOZI aliyeongoza mapinduzi nchini Guinea mwezi uliopita , Kanali Mamady Doumbouya amekula kiapo cha kuwa rais wa mpito jana na kuahidi kuheshimu wajibu wa taifa hilo kimataifa wakati wakielekea kukabidhi madaraka kwa serikali ya kiraia.
Hata hivyo kwa mara nyingine hakuzungumza chochote kuhusiana na muda atakaoongoza kama rais wa mpito na ameapa kuuendeleza kwa uaminifu uhuru wa taifa hilo.
Doumbouya aliyeongoza mapinduzi yaliyomuangusha Rais Alpha Conde Septemba 5 ameapa mbele ya kiongozi wa mahakama ya juu nchini humo Mamadou Sylla kuongoza katika kipindi hicho cha mpito huku akiapa kuuendeleza kwa uaminifu uhuru wa taifa hilo.
Hafla ya uapisho ulifanyika kwenye kasri la Mohammed-V, siku moja kabla ya kumbukumbu ya azimio la mwaka 1958 la uhuru kutoka kwa Ufaransa ambayo huwa ni siku ya mapumziko.