Ilipoishia wiki iliyopita
Nikiwa nimelala kama saa nane usiku, ghafla nikahisi joto kali chumbani na kwa uzoefu wangu wa Iringa, kipindi kile ni cha baridi. Haraka nikaamka, nikasikia harufu ya moto, nikavaa suruali haraka nikatoka nje. Kulikuwa na moshi mwingi pale kwenye korido, sikuona chochote!Sasa endelea…
Moshi ulikuwa ni mwingi sana kiasi kwamba ingawa taa zilikuwa zinawaka, lakini mwanga wake ulionekana mwekundu usiopitisha nuru yoyote. Na mlango wa chumba changu ukaanza kuingiza moshi, nikajiuliza harakaharaka, nikaamua kupiga kelele za moto, moto, moto moto!
Ilikuwa kama nimewazindua, kwani mara nikasikia milango mingine nayo ikifunguliwa na mara nyumba nzima ikawa kelele tupu. Nikapiga hesabu za namna ya kujinusuru, nikakosa, kwani katika madirisha, kulikuwa na nondo, hivyo nisingeweza kufanya lolote.
Nikasikia watu wakiwa wanavunja mlango mkubwa wa mbele ya ile nyumba na nje, zikasikika hekaheka zilizotupa matumaini watu tuliokuwa ndani. Lakini mara, watu wale wa nje wakapaza sauti kututaka kusogea karibu na mlango ili tusaidie kuufungua, kwani ulikuwa umefungwa kwa ndani na wao wasingeweza kufanya lolote.
Joto lilizidi na moshi sasa nao ukawa unaongezeka taratibu kwani nikaanza kukohoa mfululizo huku wapangaji wenzangu nao wakiendelea na vilio. Mara nikapata wazo, nilipotazama juu ya dari, nikaona sehemu ambapo kuna tundu. Nikapanda juu ya kabati la nguo na kuuvuta kwa nguvu mfuniko wa ile dari, ukajiachia.
Nikapanda juu na kufanikiwa kuingia darini. Nako kulikuwa na joto la ajabu sana, lakini nikagundua kuwa nisingeweza kufanya lolote kwa vile bati lilikuwa gumu. Nikakumbuka kuwepo kwa chuma kule chumbani, nikarudi na kukichukua kile chuma, nikarudi tena juu na kuanza kulifumua bati katika sehemu moja iliyoonekana ni maungio.
Kitu kingine cha kutisha ni kuwa bati nalo lilishaanza kupata moto, haikujulikana moto huo ulikuwa unawakia wapi. Ilibidi nijitahidi kwa sababu kama ningezembea, ningeweza kuzimia maana joto na moshi vilikuwa vinazidi kunimaliza pumzi.
Baada ya dakika kama kumi hivi, nikafanikiwa kufunua kipande cha bati hilo, nikajikaza kulishika na kujitokeza nje. Upepo wa nje ulinipa faraja kubwa, nikajitahidi kujitoa kabisa ndani. Nikiwa kule juu, nikapiga kelele kuwaambia watu kuwa nilifanikiwa kutoka kupitia kwenye paa, nao wakaniambia niambae pembeni mwa bati hilo hadi nitakapoifikia nguzo ya umeme niweze kushuka.
Nikafuata maelekezo yao huku nikiwa natetemeka, maana mabati yalikuwa ni ya moto na pia yalikuwa yanateleza hivi. Nikawa natembea nikiwa kama natambaa, nikajisogeza taratibu hadi nilipokaa karibu kabisa na nguzo.
Ghafla, mbele yangu nikaona kitu cha kutisha mno, sikukielewa kama ilikuwa ni paka, chui au mnyama gani, lakini ninachokumbuka, ni macho yake kuwa mekundu na makali. Kitu hicho kikawa kinanifuata kwa kasi.
Ili kujiokoa, nikajikuta nikiruka kutoka juu ya paa la nyumba huku nikipiga mayowe. Nahisi nilipoteza fahamu kabla ya kuanguka chini maana sikukumbuka kilichotokea.
Je, ni kitu gani kilimpata? Usikose kufuatilia mkasa huu katika toleo lijalo.