ILIPOISHIA:
Niliingia ndani na kujitupa kitandani, pamoja ilikuwa burudani lakini iliniacha hoi. Niliamka saa sita za usiku nikiwa na njaa kali. Nilipata chakula kisha nilioga na kurudi kitandani, kutokana na uchovu nilipogusa kitandani usingizi mzito ulinichukua.
Huwezi kuamini usiku mzima njozi zote zilikuwa kwa babu Sionjwi mpaka kunakucha.
SASA ENDELEA..
Niliposhtuka kitandani na kujikuta peke yangu nilijikuta nikiingia unyonge na kujilaumu kumrudisha mapema heri ningeachana naye jioni ya siku ile.
Nilitakiwa nitumie siku ile kujiandaa kwa kukaa na familia kwa ajili ya kupanga na kuagana. Siku zote safari kama ile ilitakiwa upate baraka za wazazi.
Lakini nilijikuta nikimuwaza sana babu na kutamani niwe naye karibu, niliona kuna haja ya kumfuata kisha awe mjini na kufanya akili yangu itulie na kuweza kupata utulivu wa moyo ambao niliuona kama ukipepea kutaka niwe karibu ya babu muda wote.
Kwa vile jioni ya siku ile nilikuwa na miadi ya kukutana na familia kwa ajili ya sherehe fupi ya kuniaga. Niliona asubuhi ile kuna haja ya kukimbilia kijijini kumfuata mzee Sionjwi ili niwahi kurudi kujiandaa na sherehe iliyokuwa ya kifamilia, sikutaka kubwa zaidi ya familia yangu tu.
Kumbukumbu zangu zilinionesha baada ya kupata kifungua kinywa, niliwaaga wadogo zangu huku nikiwaelekeza wanipangie nguo na vitu nitakavyoondoka navyo kwenye sanduku na begi. Kwa vile kulikuwa na dawa zilizotakiwa kuondoka nazo, niliziweka mwenyewe kwenye begi dogo ambalo ningeingia nalo kwenye ndege.
Baada ya kuacha kila kitu kipo sawa huku moyo ukinisukasuka kama mtu aliye na kiu kikali aliyeelezwa sehemu yalipo maji. Kila dakika iliyokuwa ikija mbele yangu niliona nachelewa kumuona babu kiumbe aliyeuteka moyo wangu kwa mapenzi mazito ambayo sikuwahi kuyapata katika maisha yangu.
Mwanzo nilimuona kama kiumbe wa ajabu asiye na hadhi kwangu lakini safari yetu ya mjini na jinsi alivyobadilika na kuonekana mzee wa kisasa na penzi alilonipa lilinichanganya akili mtoto wa kike.
Baada ya kila kitu kwenda kama nilivyopanga niliondoka kumfuata babu ambaye nilipanga kulala naye nyumbani kwangu na kushinda naye mpaka jioni ya kesho yake ambayo ningemkodia gari mpaka kijijini huku mimi nikielekea uwanja wa ndege kwa safari.
Niliwasha gari kuelekea kijijini kumfuata babu tustarehe kwa mara ya mwisho kabla ya kuondoka jioni ya siku ya pili. Njia nzima mawazo yangu yote yalikuwa kwa babu nilimuona kama kijana wa miaka kumi na nane kwa jinsi alivyouteka moyo wangu kwa kasi ya ajabu na kujuta kuchelewa kumfahamu.
Nilijilaumu kuchelewa kumjua babu mapema kwani mpaka naondoka moyoni mwangu ningemuona wa kawaida japokuwa ningekuwa nampenda lakini si kwa kiasi kile cha kuhisi kuchanganyikiwa vile kila nilipomuwaza.
Katika kumbukumbu zangu za mwisho, nakumbuka nilifika mpaka kwa babu na kupokelewa, lakini kilichoendelea kuanzia hapo sikuelewa chochote mpaka siku tulipofumwa na mama Sabuni.
Mama Sabuni ndiye aliyenielekeza kwa mzee Sionjwi kwa msaada wa shoga yangu Rose baada ya kusumbuliwa na mhasibu wangu Mbwana, aliyekuwa akishikilia ofisi kishirikina wakati elimu yake ilikuwa ndogo tofauti na cheo alichokuwanacho baada ya waganga wengi kugonga mwamba kumng’oa.
Alikuwa amemleta mtu aliyekuwa na matatizo ya muda mrefu hivyo alimkumbuka babu Sionjwi na kwenda kubahatisha kama yupo kwa vile ulikuwa muda mrefu tangu aende kupata huduma mara ya mwisho.
Alipofika alimfahamu shoga yangu Rose ambaye aliwahi kufanya naye kazi kabla mimi sijafika. Kwanza alimfananisha alipomwita jina lake kama ni yeye kweli.
“Rose.”
“Abee,” Rose aliitikia bila kumfahamu aliyemwita.
“Unafanya nini huku?”
“Kwani we nani?”
“Mimi mama Sabuni.”
“Mama Sabuni yupi?’
“Rose si tulikuwa tunafanya ofisi moja siku za nyuma na wewe ndiye uliyemleta shoga yako kuomba msaada nikawaelekeza huku.”
“Ooh! Za siku?” Rose alimkumbuka.
“Nzuri, Rose unafanya nini huku?” “Kwani unaniona nafanya nini?” Rose alimjibu kwa mkato huku akimtengeneza mtoto aliyekuwa mgongoni.
Itaendelea Risasi Jumamosi.