
TAMASHA kubwa duniani la Afro Nation limerudi baada ya kutofanyika kwa miaka miwili kutokana na janga la UVIKO-19 huku wasanii wakubwa kutoka nchi tofauti za Afrika wakitajwa kupafomu.
Kubwa zaidi, kutoka Tanzania, mwanamuziki wake kinara, Nasibu Abdul almaarufu Diamond Platnumz amepewa ukubwa kutumbuiza mbele ya wanamuziki wakubwa barani Afrika, Wizkid na Burna Boy kutoka Nigeria.
Tamasha hilo litafanyika kwa muda wa siku tatu huko Algarve, Portimao nchini Ureno ambapo wanamuziki hao wataoneshana umwambwa kwenye jukwaa moja.
Mastaa wote ni wakali, hakuna anayepinga uwezo wa Burna Boy licha ya ukubwa alionao ila ni mzuri kwenye jukwaa kama ilivyo kwa Wizkid na hata Megan Thee Stallion ambaye naye amejumuishwa.
Kibongobongo, hapana shaka na uwezo wa Diamond au Mondi linapokuja suala la kushika kipaza na kuwainua mashabiki jukwaani.
BURNA BOY
Burna Boy ni staa mkubwa siyo tu kwenye nchi yake ya Nigeria, bali hata kwenye nchi nyingine nje ya Bara la Afrika.
Burna Boy ni mshindi wa Tuzo za Grammy ambaye atakiwasha na Diamond.
Kwa ukubwa alionao Burna Boy siyo rahisi kutia aibu jukwaani, atataka kuonesha kuwa ni mwamba Afrika.
WIZKID
Kama ni mfuatiliaji mzuri wa muziki, basi utakuwa unaelewa balaa la Wizkid ambaye ametamba na anatamba na ngoma yake ya Essence ambayo inakimbiza huku ikiwa inashika chati katika mitandao mikubwa duniani kama Billboard.
DIAMOND
Diamond au Simba anawakilisha vyema Taifa la Tanzania nje ya mipaka na kama ni mfuatiliaji mzuri wa muziki wa kizazi kipya, basi unafahamu namna alivyovunja na kuweka rekodi za wasanii wakubwa Afrika.
Licha ya kuwa msanii pekee kutoka Tanzania, pia ni msanii pekee Afrika Mashariki kuitwa kupafomu katika tamasha hilo kubwa litakalofanyika mwakani 2022.
UKUBWA WA DIAMOND
Kama kuna maswali juu ya ukubwa wa Diamond kwenye muziki, basi maswali hayo yatapata jibu sahihi mwaka 2022 baada ya kupafomu katika jukwaa la Afro Nation litakalokuwa na mastaa wakubwa kama hao.
Kwa waliohudhuria shoo zake wanasema hawana shaka na uwezo alionao Diamond linapokuja suala la kushika kipaza sauti na kuwafurahisha mashabiki kwani ana kipaji kikubwa cha kutawala jukwaa.
Diamond ana ‘vibe’ na anaweza kwenda sambamba na mashabiki.
Jamaa huyo ana uwezo mzuri wa kutumia mwili wake kucheza na anaweza kuzunguka jukwaa zima akamridhisha kila aliyehudhuria kwa namna anavyopafomu.
Siku za hivi karibuni, staa huyo wa kimataifa, amekuwa akifanya shoo za nje huku akionesha balaa lake.
Katika Tamasha la Afro Africa nchini Ureno, Diamond atataka kuonesha nini anamaanisha akisema yeye ni Simba.
DIAMOND KUWAPA ZA USO
Kwa uwezo alionao, Diamond ndiye anatajwa kuwa ataibuka kinara kwenye tamasha hilo na kuwagaragaza Burna Boy na Wizkid.
STORI; BAKARI MAHUNDU, DAR