
STAA wa muziki kutoka WCB Wasafi, Raymond Shaban maarufu kama Rayvanny ameweka wazi taarifa za ujio wa ziara ya tamasha maalumu kwa ajili ya msanii wake mpya kutoka kwenye Lebel yake ya Next Level Music (NLM).
Rayvanny amebainisha hilo kupitia ukurasa wake wa mtandao wa Instagram (Insta Story) kwa kuandika maneno yanayosomeka “Macvoice Tour… Show Time”, maneno ambayo yanaashiria kuwa wasaa wa msanii huyo kuanza ziara yake ya kwanza tangu kutambulishwa kwake umefika rasmi.
Mac Voice ni msanii mpya na wa kwanza kutambulishwa chini ya Lebel ya muziki inayomilikiwa na msanii Rayvanny takribani mwezi mmoja uliopita akiachia Extended Playlist (EP) iitwayo “Voice” yenye jumla ya nyimbo sita.
Na hivi karibuni ametajwa kuwania tuzo ya African Entertainment Awards USA 2021, kupitia kipengele cha msanii bora anayechipukia kwa mwaka 2021 akishindana vikali na wasanii wengine kutoka nchi kadhaa barani Afrika akiwemo Oxlade, Liya Guchi, Ayra Starr na Omah Lay.