×

Lava Lava Iwe Funzo Kwake na Wengine

MWAKA 2017 ndipo Lava Lava alianza kusikika kupitia ngoma zake akiwa kwenye lebo kubwa ya muziki Bongo ya Wasafi Classic Baby (WCB).

Lakini safari yake ya muziki ilianza kabla ya hapo akiwa pale Nyumba ya Kukuza Vipaji (THT) ambapo bado hakusikika kiivyo.

 

Lava Lava amesikika kwenye ngoma nyingi na kali zilizofanya wandaz kama Go Gaga, Tuachane, Niuwe, Gundu, Walewale na nyingine zilimfanya asifiwe kiaina mitaani.

 

Mwaka mmoja baadaye Mbosso akatia maguu WCB, akapiga Hodari, akafyatua Nadekezwa, akatoa Tamu basi akazidi kuwa mtamu pale Wasafi ambako msanii mkubwa Bongo, Diamond Platnumz ndiye bosi wa lebo hiyo.

 

Aprili 2020, Zuchu naye aliingia anga za WCB, akapiga zake, Nisamehe, akagonga Wana, akaachia Litawachoma, halafu akatoa Sukari na tangu hapo akawa anayelambwa karibu kila mtaa.

Swali likawa ni kwa nini Lava Lava ameshindwa kufurukuta mbele ya Mbosso na Zuchu ndani ya WCB pamoja na kwamba ana kipaji kikubwa?

 

Wachache wanamtania kwenye mitandao ya kijamii kuwa huwezi kuimba Gundu halafu ukategemea kupata bahati.

Ina maana Lava Lava ana gundu WCB? Swali linakuwa gumu, ingawa kwa mbali unaweza kusema analo kweli kutokana na nini ujue? Havumi kama wenzake.

 

Hata bosi wake, Diamond amekuwa kando mno na yeye kwenye kufanya naye kolabo. Unajiuliza kwa nini anamtenga msanii huyo tofauti na Mbosso na Zuchu ambao ameshirikiana nao kwenye ngoma kibao?

Bila shaka kuna siri nzito katika jambo hili na mfumbua siri hiyo akawa anabaki kuwa ni Lava Lava; pengine siku zikitimia atakuja kusema jambo lililo nyuma ya pazia katika safari yake ya muziki.

 

Ila kusema kweli Lava Lava hakupaswa kuchukuliwa poa, kwani ngoma zake zimekuwa zikifanya vizuri, hata ile ya Nikomeshe bado inakimbiza mjini YouTube, ingawa siyo kwa kasi kubwa.

Lakini Lava Lava anafahamika ni mtunzi mzuri sana wa ngoma za mapenzi. Pia amebarikiwa sauti nzuri na hilo linafahamika.

 

Tatizo la huyu jamaa inasemekana ni mvivu wa kutupwa, kuna waliosema amebweteka, haendani na wakati; yaani kifupi alionekana tofauti na wasanii wengine wa Wasafi. Kila mtu akawa anauliza kwani Lava Lava anakwama wapi? Mbona yupo sehemu salama tu? Sehemu ambayo ni kubwa ambayo kama asipolala, atakuwa mbali sana?

 

Hivi tujiulize, Lava Lava anakubalije Mbosso ampite wakati yeye ndiye alitangulia Wasafi? Mbona Mbosso anamzidi mafanikio? Mbosso anapiga shoo kubwa kuliko yeye, tatizo likawa amebweteka na haendani na kasi ya muziki ya sasa.

 

Kwangu nikasema hapa, namuona Lava Lava ana kipaji kikubwa kikubwa sana na sehemu aliyopo ni kubwa; WCB.

Kitu pekee nilichokiona kinamfelisha ni jitihada tu, ajitume kama wanavyojituma wengine kwani ninavyojua tatizo halikuwa kwa uongozi, tatizo lilikuwa kwake mwenyewe; ilikuwa ni kiasi cha kuamka tu na kukimbiza kinoma.

 

Na hicho ndicho amekifanya wiki kadhaa zilizopita ambapo aliachia ngoma ambayo inamsuta na kumuonesha kuwa kuna mahali ambapo alikuwa hajapafikia bado.

Wiki tatu zilizopita aliachia Ngoma ya Inatosha na kweli imetosha kwa sababu namba zake kwenye platforms mbalimbali zinajieleza.

 

Kwa mara ya kwanza, Lava Lava kupitia ngoma hiyo amejikusanyia views zaidi ya milioni 2 kwenye YouTube ndani ya muda mfupi; ngoma zake nyingine zilizshindwa kufanya hivyo.

Ngoma hiyo inazungumzia mhusika kukata tamaa katika mapenzi baada ya kupitia maumivu na ugomvi kwenye mahusiano.

 

Kwa mujibu wa mashairi ya ngoma hiyo, ugomvi unapozidi na kuwa mwingi kwenye mapenzi, basi ni heri mtu ajitoe au akae pembeni ili apate utulivu wa akili. Jina la ngoma hiyo linatokana na mhusika ambaye kwenye ngoma hiyo ni Lava Lava mwenyewe, akikata kauli kuwa maumivu aliyopitia kwenye mapenzi yametosha na basi ni wakati wake kuchukua mkondo mpya.

 

Lava lava pia anasema kuwa upendo wa wazazi wake unatosha na hahitaji upendo zaidi.

“Sasa nimekua, nimejua mapenzi uchizi. Yule unayempenda ndo anakunyima usingizi. Kwake moyo unautua bila ikipingamizi. Na kesho anakuzingua mapenzi ya siku hizi. Unatuma meseji mchana anajibu usiku. Unatuma meseji usiku anajibu mchana. Unatuma meseji mchana anajibu usiku. Mapenzi unamwona online anachati na kukujibu hataki. Anaposti yuko kwa parti na marafiki,” anaimba Lava Lava kwenye Inatosha.

 

Video ya ngoma hiyo imefanya na Hanscana ambaye pia ni mwelekezaji wa video za wasanii wa WCB. Video hiyo ni ya kipekee kama vile ngoma yenyewe kwani wazo lake limeleta muziki wa kale na wa kizazi kipya pamoja.

 

Aidha, ngoma hiyo imesifiwa kutokana na kuleta ladha ya mtindo wa Rhumba na wa Bongo Fleva pamoja. Hii imeonekana kama ubunifu wa kipekee kwenye sanaa ya muziki, kwani ni vigumu kujumuisha mitindo miwili kwa pamoja na mwisho wa siku ukapata ngoma nzuri kama ya Inatosha ya Lava Lava.

Kwa kilichotokea na sasa kila mtu anampongeza, basi liwe ni somo kwake Lava Lava na wasanii wengine wajifunze kwake!

MAKALA; SIFAEL PAUL, BONGO

Leave a Comment