
Benki ya Maendeleo ya Kiarabu (BADEA) imeahidi kuipatia Tanzania mikopo yenye masharti nafuu pamoja na misaada inayokadiriwa kufikia dola za Marekani bilioni 3 sawa na Sh trilioni 7 katika kipindi cha miaka mitano ijayo kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.
Ahadi hiyo imetolewa Jijini Cairo Nchini Misri na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo Dk. Sidi Ould Tah alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Lameck Nchemba.
“Tumekuwa na majadiliano ya kina na yenye tija na Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango wa Tanzania pamoja na ujumbe wake ambapo tumejadili mambo mengi ya msingi kwa ajili ya uhusiano wetu kama Benki na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na tuko tayari kutoa fedha hizo” alisema Dkt. Tah.
Alifafanua kuwa fedha hizo zitatolewa katika kipindi cha miaka 5 ya utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo katika maeneo matano ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya barabara, elimu, kilimo, kuimarisha sekta binafsi pamoja na kuwajengea uwezo wataalam.