
KAMPUNI ya Kuhifadhi Mafuta Tanzania (TIPER), imesema upo wezekano wa kudhibiti kupanda kwa bei za mafuta ya petroli na dizeli kila mara iwapo Serikali itaridhia kutumika kwa miundombinu ya kampuni hiyo kuhifadhi mafuta yote yanayoingizwa nchini kwa pamoja.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Naibu Meneja Mkuu wa TIPER, Martin Mosha amesema kampuni hiyo inauwezo wa kutosha kuhifadhi mafuta ya makampuni mbalimbali yanayoagiza nishati hiyo.

Amesema tangu kuanzishwa kwa TIPER mwaka 1999, kumekuwepo na maboresho mbalimbali ambapo awali ilikuwa na uwezo wa kuhifadhi lita milioni 140, mwaka 2015 – lita milioni 212 lakini sasa TIPER baada ya kufanya maboresho makubwa ya miundombinu yake ina uwezo wa kuhifadhi lita milioni 253.6 sawa na milioni 254.

Amesema kutokana na uwezo huo, iwapo Serikali itaagiza mafuta yote yanayoingizwa nchini yahifadhiwe TIPER, hilo litasaidia kwanza kupunguza kupanda kwa bei ya mafuta kwani pindi mafuta yakishuka makampuni ya uagizaji yakishanunua kwa wingi yatakuwa na uhakika wa kuwa na sehemu ya kuhifadhi kiasi kikubwa cha mafuta hapo TIPER na pale yatakapopanda, kiasi hicho kilichohifadhiwa kitaanza kutumika.
“TIPER inao uwezo kwani inayo leseni ya kuhifadhi mafuta hayo yatakayoingizwa nchini kwa pamoja,” amesema.
“Ameendelea kusema kuwa uamuzi huo utasaidia kupunguza makali ya kupanda kwa bei ya mafuta nchini”.
“Lakini pia kwa kuwa hapa tuna miundombinu yote ya mafuta kwamba, kila kampuni iliyopo nchini, inayojihusisha na biashara ya kuagiza mafuta, ina bomba lake linalopitia hapa TIPER ambalo sasa kama mafuta ya kampuni husika yakihifadhiwa hapa Serikali itakuwa na uwezo wa kupata kodi kwa uhakika na usahihi zaidi.
“Pia upotevu wa mafuta utapungua, kwa sababu ni jambo la kawaida mafuta kidogo kupotea kwenye mabomba lakini kuna kiwango maalumu kinachokubalika kimataifa, hivyo ili kupunguza mzunguko mkubwa mafuta yakihifadhiwa hapa hakutakuwa na mzunguko mrefu kurahisisha mafuta kupotea,” amesema.
Pia ameongeza kuwa TIPER inazo ‘flow meter’ sita zinazotumika kupima mafuta kwa kiwango kinachotakikana kimataifa.
“Tunayo mapipa 33, lakini yanayotumika ni 32, kwa hiyo uwezo wa kutoa tunao, na hata suala la usalama ni jambo lingine ambalo tumewekeza pakubwa ndio maana ni nadra sana kusikia ajali za moto katika eneo hili la TIPER,” amesema.
Amesema yapo makampuni yenye miundombinu ya kuhifadhi mafuta yake yenye yenyewe lakini kwa Tanzania, TIPER ndio yenye miundombinu bora, mikubwa na sahihi kwa uhifadhi wa mafuta hayo.
Amesema TIPER inamilikiwa kwa asilimia 50 na Serikali pamoja na Kampuni ya Oryx Energy ya Geneva inamilikia asilimia 50 zilizobaki.
“Hata mwenyekiti wa bodi ya Tiper anateuliwa na rais, hivyo hapawezi kuwa na wasiwasi wowote kuwa TIPER sio chombo cha Serikali, hili ni jambo ambalo tumefanya vikao mara kadhaa lakini bado halijatolewa uamuazi,” amesema.
Amesema katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, TIPER imetoa gawio kwa Serikali la Sh bilioni 28, pia imekusanya mapato ya Sh bilioni 62.