×

Damu Changa Noma, Wamekiwasha ile Mbaya

WAKATI tukielekea ukingongoni kabisa wa mwaka, kama kuna mwaka kwenye historia ya muziki wa Tanzania ambao wasanii wapya wamepata nafasi ya kusikika na kuonesha vipaji vyao mbele ya Watanzania, basi mwaka 2021 umeweza kufanya hivyo vizuri sana.

 

Kuanzia Januari hadi Desemba mwaka huu, ifuatayo ni listi ya wasanii chipukizi wa muziki Tanzania ambao wamekiwasha ile mbaya.

 

ANJELLA

Mashabiki wa Bongo Fleva walimfahamu baada ya kushirikishwa na Harmonize kwenye Ngoma ya All Night ambayo aliitendea haki na kila shabiki wa muziki akatamani kumjua na kumuona tena na tena; wengi walitamani kumuona tena kwenye ngoma nyingine hasa akiwa mwenyewe bila kushirikishwa ili kujua yaliyomo yamo?

 

Tangu hapo malkia huyo wa Lebo ya Konde Gang akaanza kuachia muwa baada ya muwa zikiwemo Kama, Sina Bahati, Nobody na nyinginezo na sasa amejitengenezea kijiji chake cha mashabiki na kuweka rekodi ya kusikilizwa na kutazamwa kwenye mitandao inayodili na muziki duniani.

 

SARAPHINA

Saraphina alianza kusikika miaka miwili iliyopita baada ya kujirekodi akiimba ngoma za wasanii wakubwa kama Diamond Platnumz, Rayvanny, Vanessa Mdee na Teni. Mwaka 2021 ndiyo Tanzania ilimfahamu vyema Saraphina baada ya kuachia ngoma zake kama In Love, Sitaki Tena na Siyo Kitoto akiwa ameshirikishwa na wasanii wakubwa kama Chege na Baddest 47.

 

LODY MUSIC

Mwamba huyu ambaye pia ni mwanachuo alitetemesha Tanzania na ngoma yake ya Kubali ambayo imemfanya kufahamika na Watanzania. Hadi Desemba, ngoma hiyo imetazamwa mara zaidi ya milioni 1.1 kwenye Mtandao wa YouTube.

 

MAC VOICE

Tangu ajiunge na Lebo ya Next Level Music ya Rayvanny, Mac Voice amekuwa msanii mkubwa, hasa baada ya kuachia EP yake ya My Voice ambayo imesheheni ngoma sita. Wiki chache baada ya kuzinduliwa EP hiyo, Mac Voice alitajwa kuwania Tuzo za AEUSA 2021 katika Kipengele cha Msanii Bora Chipukizi Afrika.

 

ROSE NDAUKA

Pamoja na kwamba ni mkongwe kwenye Bongo Movies, lakini kunako Bongo Fleva alionekana ni chipukizi. Pamoja na kuambiwa hajui kuimba, lakini Rose ametisha mno 2021 na ngoma zake kama Sijali, Makiki, Ghost Freestyle na nyinginezo ambazo zimejikusanyia wasikilizaji na watazamaji lukuki kwenye mitandao ya muziki.

 

ABBY CHAMS

Abby Chams ameweza kujijengea jina kubwa kwenye muziki wa Tanzania kwa kutumia sauti yake ya kuvutia. Chams ameweza kutoa ngoma tofauti kama Chapa Lapa, Tucheze na nyinginezo. Ngoma yake kubwa kabisa ni ile ya Kings Of Kings ambayo amefanya na Darassa.

 

HANSTONE

Baada ya tetesi za muda mrefu kuwa amesainiwa kwenye Lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB), ilipofika Oktoba 7, mwaka huu, Hanstone alifutilia mbali tetesi hizo baada ya kuachia EP yake ya Amusing ambayo ina ngoma sita. Hata bila kushikwa mkono na lebo yoyote, EP ya Hanstone imefanya vizuri kwenye mitandao mbalimbaliya muziki.

 

SENETA KILAKA

Wabongo walimfahamu zaidi baada ya Hamisa Mobeto kufanya remix ya ngoma yake ya Ex Wangu. Kutoka hapo, Seneta Kilaka hajawahi kurudi nyuma kwani mwezi Septemba mwaka huu aliachia EP yake aliyoipa jina la King of Singeli ambayo imezidi kuthibitisha ubora wake kwenye muziki wa Singeli.

 

FRIDA AMANI

Mwaka 2021 kipaji cha Frida Amani kilionekana kupitia ngoma yake ya Madam President ambayo ilisikika kila kona ya nchi na kumpatia ubalozi wa kampeni mbalimbali za Serikali ya Tanzania.

 

AGGY BABY

Kwa mara ya kwanza mrembo Agness Suleiman almaarufu Aggy Baby kutoka Bongo Movies alisika rasmi kunako Bongo Fleva. Amekimbiza na ngoma zake kama Wanipa na Watajuaje na kuonesha nyota njema huko mbeleni.

MAKALA; SIFAEL PAUL, BONGO

Leave a Comment