
WAZIRI wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (MB) amefanya ufunguzi wa jukwaa la wadau wa sekta mtambuka ambalo limewahusisha wadau wakubwa wa matumizi ya Maji Bonde la Wami Ruvu lililofanyika Mkoani Morogoro.
Aweso amesisitiza Bonde la Wami Ruvu kuhakikisha kazi kubwa inafanyika kulinda na kutunza vyanzo vya Maji ikiwa ni pamoja na kuishirikisha jamii ili kupata ushirikiano na kufikisha elimu ya utunzanji wake ikiwa ni pamoja na usimamizi wa sheria.
Katika hatua nyingine Aweso amewakumbusha hali iliojitokeza karibuni kwa kupungua kwa kina cha maji chanzo cha Wami Ruvu na kusisitiza kuwa hili ni funzo kubwa juu ya utunzaji wa Mazingira na vyanzo vya Maji na kuhitimisha kuwa hali kama ile kutojitokeza tena.
Aidha, Waziri Aweso ametoa wito kwa mamlaka za mabonde nchini akihimiza wataalam kutumia taaluma zao vilivyo kuisaidia jamii hasa kwa kutambua na kutafiti kwa kina maeneo yenye maji akionesha ushuhuda wa maeneo yaliosemekana hayana maji chini ya ardhi na baada ya msisitizo wake maji yamegundulika kwa wingi.
Mhe Aweso amekabidhi pikipiki nne kwa wenyeviti na makatibu wa jumuiya za watumia maji wa bonde dogo la mto Ngerengere, Wami, Mkondoa Mashariki, na Mkondoa kati pamoja na mifuko 100 ya simenti Kwa ajili ya ujenzi wa madarasa katika shule ya msingi Msolwa na kusisitiza pikipiki hizo zikafanye kazi husika na sio vinginevyo.