
Rais Samia Suluhu Hassan amesema lazima nchi ikope kwaajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ikiwamo ujenzi wa madarasa kwa kuwa fedha za tozo haziwezi kutosheleza mahitaji ya miradi hiyo.
Mkuu huyo wa nchi ametoa maelezo hayo leo Jumanne Januari 4, 2021 Ikulu ua Dar es Salaam wakati wa kupokea taarifa ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uviko-19.
Amesema kuna mahitaji wa madarasa mengi katika sekta ya elimu ambayo kwa kutegemea fedha ya tozo itachukua muda mrefu kukamilisha mahitaji hayo.
“Lakini ndugu zangu tulichopata hapa leo zaidi ya fedha hizo za Uviko-19, kuna fedha ya tozo ambayo na yenyewe ilipoanza ilipigiwa kelele eee, tukasema ngoja tupunguze tukapunguza, baada ya kupunguza kelele zimeshuka” amesema Rais nakuongeza.
“Lakini wapigaji kelele hao wa sasa hivi waliuliza kuna fedha ya tozo kwa nini tunakwenda kukopa”
Amesema mpaka sasa fedha zilizopatikana kwenye tozo zimejenga madarasa 5,00 lakini uhitaji wa ni zaidi ya madarasa 10,000 kwa shule za msingi pekee.
“Takwimu zilizotolewa na mawaziri hapa zinatosheleza kwamba pamoja na kwamba tuna fedha za tozo mahitaji ya madarasa shule za msingi ni 10,000 mpaka sasa hivi, tumeweza madarasa 5,00 kwa fedha za tozo, tunafika lini? Amehoji Rais Samia na kusisitiza.
“Lazima tukope tuweke miundombinu”
Amesema kuna uhitaji mkubwa wa madarasa kwa siku zijazo hivyo kutegemea fedha ya tozo itachelewesha kufikia malengo kwa wakati.
“Tuna madarasa mbele yanahitajika, tunayajenga kwa fedha za tozo kweli?, ambayo mpaka sasa imetusaidia madarasa 5,00, hatuwezi kwenda na fedha ya tozo”
“Kwa hiyo inashangaza kuona mtu mwenye uelewa anasema kuna fedha ya tozo lakini kaenda kukopa ya nini au kwa nini tunaendelea kutoza tozo wakati fedha ya mkopo ipo” amesisitiza.