
JAPAN na Marekani zimewataka watu wanaoishi kwenye mwambao wa bahari ya Pasifiki kuhama na kwenda sehemu za miinuko, kutokana na kitisho cha Tsunami baada mlipuko wa volkano ya chini ya bahari karibu na kisiwa cha Tonga.
Picha za satelaiti zimeonyesha mlipuko wa volkano hiyo ya Hunga Tonga-Hunga Ha’apai, ambao umerusha angani moshi na majivu katika umbo la uyoga mkubwa, na kusababisha tetemeko katika eneo la bahari ya Pasifiki linalokizunguka kisiwa cha Tonga.
Taarifa za taasisi ya hali ya hewa ya Australia zinasema mawimbi yenye kima cha mita 1.2 yalishuhudiwa katika mji mkuu wa Tonga wa Nuku’alofa.
Japan pia imeripoti kuwa mawimbi yaliyotokana na tsunami hiyo yamefika kwenye pwani yake, yakiwa na kima cha hadi mita tatu.