×

Familia Yataka Muuaji wa Mtoto Wao Aachiwe

FAMILIA ya marehemu Ally Khalifa Bakari, mtoto mwenye umri wa miaka (9) aliyefariki kwa kupigwa na kitu chenye ncha kali kichwani na mtoto mwenzake, Omari Hassan imeiomba Serikali imwachie huru mtoto huyo.

 

Mtoto huyo (Omari Hassan) ambaye naye ana umri wa miaka (9) mkazi wa mji mpya Msalo Hale na mwanafunzi wa Shule ya Msingi Kichangani, darasa la tatu iliopo wilayani Korogwe mkoani Tanga, anatuhumiwa kwa kosa la mauwaji ya Ally Khalifa aliyekuwa akisoma naye darasa moja.

 

Taarifa iliyotolewa na familia hiyo imesema kilichotokea ni makosa ya kibinadamu hivyo wameiomba Serikali na vyombo vya dola vimwachilie huru mtoto huyo.

 

Msemaji wa Familia hiyo, Adriano Petro amesema kuwa ingawa mtoto wao amefariki, kilichotokea ni mapenzi ya Mungu kwa kuwa watoto hao walikuwa wakicheza pamoja siku zote na ikatokea bahati mbaya Januari 28, mwaka huu wakiwa wanatokea Msikitini njiani wakagombana na kupigana hadi kupelekea Ally kufariki wakati akipelekwa Hospitali.

 

Mariam Hassan ambaye ni Mzazi wa mtoto anayetuhumiwa kwa mauaji (Omari Hassan) ambapo amesema amepokea tulio hilo kwa masikitiko na kuiomba Serikali kusimamia suala la elimu kwa Mtoto wake wakati huu ambapo anashikiliwa.

 

Mwenyekiti wa Kijiji cha Hale Venusi Msonela amesema wao kama Serikali wamekaa na familia za pande zote mbili ili kuondoa hali yoyote ya taharuki ambayo ingeweza kujitokeza.

 

RPC wa Tanga Sofia Jongo amesema mtoto huyo bado anashikiliwa huku akitoa wito kwa wazazi kutowaonesha watoto picha ama video ambazo haziendani na umri wao kwa kuwa wanachojifunza hutaka kufanya kwa vitendo.

Leave a Comment