×

Mastaa Waliooa Pisi Kali

ASILIMIA kubwa ya vijana wanaamini kuwa wasichana wazuri ni nadra sana kuolewa au kupata mume wa kueleweka kutokana na sababu wanazozijua wao.

 

Wapo ambao wanadai kuwa mwanamke akiwa mrembo kupitiliza; siku hizi wanaitwa pisi kali, basi humsumbua sana mwanaume kwa kuringia uzuri huo ndiyo maana wengi wao huishia kutumiwa tu na kuachwa.

Lakini pia wapo wanaume ambao huamini tu kuwa, wakioa wanawake wazuri, basi watapata shida ndani ya ndoa kwa kuhisi mke anaweza akatamaniwa na kila mwanaume, hivyo huamua tu kuoa mwanamke wa kawaida ambaye ndiye huamini anammudu.

 

Kwa kiasi f’lani naweza kupingana na dhana hii kuwa mwanamke mzuri haolewi, ina maana wasichana wazuri wote ni wa kuchezewa tu na kuachwa? Au wanamaanisha wanawake wote walioolewa ni wabaya? Jibu linakuja siyo kweli, mara nyingi tabia ya mtu ndiyo humfanya awe hivyo alivyo.

Lengo la makala haya ni kutaka kukuletea listi ya baadhi ya warembo (pisi kali) ambao wameolewa na mastaa na kutulia kwenye ndoa zao na siyo kutulia tu, lakini hata waume zao machoni pa watu wanaonekana ni watu wenye furaha na wake zao;

 

AY- REMMY

Ni msanii mkubwa wa Bongo Fleva na Afrika kwa jumla. Jina lake halisi ni Ambwene Yesayah. Mwaka 2018 aliachana na ubachela, akavuta pisi moja hatari ijulikanayo kwa jina la Remmy kutoka nchini Rwanda.

Mpaka sasa tunavyoongea ni mwaka wa nne wapo kwenye ndoa huku wakiwa wamebarikiwa mtoto mmoja wa kiume.

 

KING KIBA -AMINA

Miaka kadhaa huko nyuma, Mfalme wa Bongo Fleva, Ali Saleh Kiba au King Kiba naye aliamua kuachana na mambo ya vijana kwa kuvuta jiko, ambapo alioa mtoto mkali kutoka nchini Kenya ajulikanaye kwa jina la Amina Khaleef na mpaka sasa wameshabarikiwa watoto wawili wa kiume.

 

MC PILIPILI -CUTE

Miongoni mwa ndoa zilizotikisa vilivyo Bongo miaka ya nyuma kidogo ni pamoja na ndoa ya mshereheshaji maarufu Emmanuel Mathias au MC Pilipili ambapo kwa sasa anamiliki mtoto mkali aitwaye Philomena Thadei au Cute Mena.

Wawili hao wamejaaliwa mtoto mmoja wa kike aitwaye Elphina na siku chache zilizopita walirasimishwa rasmi kuwa wachungaji.

 

MR BLUE -WAHEEDA

Rapa mkali wa wakati wote Bongo, Kheri Sameer au Mr Blue Byser Bablon naye hakubaki nyuma kwani baada ya kubwagana na aliyekuwa mpenzi wake Najma aliamua kumuoa mpenzi wake wa muda mrefu anayejulikana kwa jina la Waheeda na sasa wamejaaliwa watoto watatu nab ado wanadunda kwenye ndoa yao.

 

GABO -TIFFAH

Staa wa filamu Bongo, Salim Ahmed almaarufu Gabo, mwaka mmoja uliopita naye alifunga ndoa takatifu na mchumba wake aliyejulikana kwa jina la Tiffah ambaye kwa kumuangalia ni kisu hasa na sasa wamejaaliwa mtoto mmoja wa kiume.

Kwa mujibu wa Gabo, licha ya kwamba mke wake ni mrembo kupitiliza, lakini ni mwanamke mwenye maadili mema hivyo kitu kikubwa anachokipenda kutoka kwake ni heshima na namna anavyomtii.

 

NIKKI WA PILI -JOAN

Rapa mkali kutoka kwenye Kundi la Weusi ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Wilaya (DC) wa Kisarawe, Nickson Simon almaarufu Nikki wa Pili anaingia kwenye orodha ya mastaa waliooa pisi kali na kuweza kudumu nayo mpaka sasa.

Kiongozi huyo anamiliki mwanamke mzuri na msomi ambaye kwa Waingereza wangesema beauty with brain aitwaye Joan Tem na tayari wamejaaliwa mtoto mmoja wa kike anayeitwa Zurii.

 

HITIMISHO

Siyo kweli kwamba mwanamke akiwa na muonekano mzuri, basi hafai kuwa mke bora ndani ya nyumba (japokuwa siyo wote). Pia itapendeza dhana hii ya kwamba mwanamke mzuri haolewi, ipuuzwe mara moja kwa sababu tumeshuhudia wanawake wengi wazuri wakiwa kwenye ndoa zao yapata miaka hata zaidi ya 10 na wanawaheshimu na kuwajali waume zao.

Tabia mbaya kwa wasichana wachache isifanya ikaharibu wanawake wote na kuonekana hawafai kuwa wake za watu. Itoshe kusema kwamba wanawake wazuri wana uwezo mkubwa wa kuolewa ila inategemea na tabia ya mtu na jinsi alivyolelewa.

Makala: Memorise Richard, Bongo

Leave a Comment